Nuru FM
Nuru FM
28 October 2025, 12:34 pm

“Lengo la mafunzo hayo ni kuwaona wanahabari katika ngazi ya kitaifa wakiweza kuhabarisha jamii juu ya mkutano huo kwa kuandika habari za kabla, wakati na baada ya mkutano”
Na Joyce Buganda
Wanahabari wametakiwa kuandika habari zenye kufikia jamii hasa katika kipindi hiki kuelekea mkutano wa umoja wa mataifa wa mabadiliko ya tabia nchi (COP 30) unaotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 10 mpaka tarehe 21 mwezi Novemba mwaka 2025 katika mji wa Belem nchini Brazil.
Akizungumza baada ya mafunzo ya siku 3 kwa wanahabari 20 kutoka mikoa 13 ya Tanzania bara yaliofanyika katika hotel ya PH EXECUTIVE iliyopo mjini Morogoro Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Media Foundation Dkt. Dastan Kamanzi amesema wanatamani kuona uandishi wenye Tija katika vyombo vya habari hasa katika suala la mabadiliko ya tabia nchi.

Awali Meneja Muwezeshaji kutoka shirika la Climate Action Network Tanzania Boniventure Mchomvu amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwaona wanahabari katika ngazi ya kitaifa wakiweza kuhabarisha jamii juu ya mkutano huo kwa kuandika habari za kabla, wakati na baada ya mkutano.
Nao baadhi ya wanahabari waliopata mafunzo hayo wamesema mafunzo hayo yamekuwa nguzo muhimu watafahamu mengi zaidi kimataifa yatakayozungumzwa katika mkutano huo wa COP 30 na kulinganisha na mambo ya nchini Tanzania ambayo yatamgusa hata mwananchi wa chini katika sekta ya mabadiliko ya tabia nchi.
Mafunzo hayo yaliandaliwa na Tanzania Media Foundation (TMF) kwa kushirikiana na Oxford policy Management (OPM) kwa ufadhili wa Ubalozi wa nchi za Uingereza na Uswisi.