Nuru FM
Nuru FM
18 October 2025, 8:56 am

“Wanahabari wakielimishwa kuhusu rushwa watatusaidia kutoa elimu kwa wananchi” Swela
Na Joyce Buganda na Adelphina Kutika
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Iringa imeendesha mafunzo maalum kwa waandishi wa habari ili kuwajengea uwezo wa kuelimisha jamii na kuripoti vitendo vya rushwa kuelekea uchaguzi mkuu.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo ya siku moja yaliyofanyika katika ukumbi wa mkoa wa Iringa Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Iringa Bwana victor Swela amewataka waandishi wa habari kutambua nafasi yao muhimu katika mapambano dhidi ya rushwa, hasa katika kipindi nyeti cha uchaguzi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Kheri James amewahimiza waandishi hao kuhakikisha wanaripoti viashiria vyovyote vya rushwa mara moja, akisema rushwa ni adui wa maendeleo na haina nafasi katika jamii inayotaka kupiga hatua kimaendeleo.
Naye Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa (IPC), Frank Leonard, ameipongeza TAKUKURU kwa kuandaa mafunzo hayo, huku akisisitiza kuwa taasisi hiyo ina jukumu la kuhakikisha waandishi wanajengewa uwezo wa kutosha ili waweze kuripoti kwa ufanisi habari zinazohusu uchaguzi na vitendo vya rushwa.
Hata hivyo mafunzo hayo yanatarajiwa kuwapa waandishi mbinu, maarifa na miongozo ya kisheria kuhusu namna ya kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa, hasa katika muktadha wa uchaguzi unaotarajiwa kufanyika nchini October 29 mwezi huu.