Nuru FM
Nuru FM
23 September 2025, 8:00 pm

Na Adelphina Kutika
Madaktari bingwa wapatao 45 kupitia mpango wa Rais Samia Suluhu Hassan wamewasili katika Mkoa wa Iringa kwa lengo la kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakilazimika kusafiri nje ya mkoa iringa kufuata matibabu.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amesema ujio wa madaktari hao utasaidia kupunguza gharama za wananchi kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma katika hospitali za kanda na mikoa mingine.
Naye Mratibu wa zoezi hilo kutoka Wizara ya Afya Dkt. Mac Donald Ulimbakisye amesema wamejipanga kutoa huduma kwa ufanisi mkubwa kwa wagonjwa watakaojitokeza katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dkt. Sylivia Mamkwe amesema huu ni ujio wa awamu ya nne ya madaktari bingwa mkoani humo, ambapo katika awamu ya tatu zaidi ya wananchi elfu mbili walifikiwa na huduma hizo.
Hata hivyo huduma hizo zinaanza kutolewa September 22 hadi tarehe 26 2025 katika hospitali za wilaya zilizopo katika Halmashauri tano za mkoa wa Iringa zikijumuisha fani saba za kibingwa ikiwemo magonjwa ya wanawake na uzazi ,Magonjwa ya ndani,Magonjwa ya kinywa na meno na Upasuaji