Nuru FM
Nuru FM
22 September 2025, 10:28 am

“Habari zisizo na maadili huleta taharuki katika Jamii”DC Sitta
Na Adelphina Kutika
Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Mhe. Benjamin Sitta, amewaagiza waandishi wa habari kutumia mitandao ya kijamii kwa kuandika na kusambaza habari zenye tija kwa jamii, na si zile zinazopotosha umma au kuleta taharuki.
Wito huo umetolewa katika mkutano wa majadiliano kati ya Baraza la Habari (MCT), waandishi wa habari, na maafisa wa serikali, Sitta amesema kuwa mitandao ya kijamii ni silaha yenye nguvu inaweza kujenga au kubomoa, hivyo, waandishi wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha matumizi sahihi ya majukwaa hayo.
Kwa upande wake Afisa kutoka MCT Ziada kilobo amesema majadiliano hayo yamelenga kujadili changamoto zinazowakabili waandishi wa habari, pia kubainisha haki na wajibu wa pande zote zinazohusiana na tasnia hiyo, ili kuweka mizani sawa kati ya waandishi wa habari na mamlaka za serikali.
Awali Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa (IPC), Frank Leonard, amesema wanahabari wanakumbana na madhila mbalimbali ikiwemo hofu inayozuia sauti ya ukweli wa jamii na kupunguza imani ya wananchi kwa vyombo vya habari.
