Nuru FM
Nuru FM
27 August 2025, 1:05 pm

Matumizi ya nishati safi ya kupikia yanalenga kupunguza athari za kiafya, mazingira na kuboresha maisha ya wananchi, huku ukipunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
Na Adelphina Kutika
Katika juhudi za kuhimiza matumizi ya nishati safi na kuboresha lishe katika jamii, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepongezwa kwa uongozi wake thabiti na dira inayolenga kuwaokoa wanawake kutoka kwenye madhara ya kiafya yanayosababishwa na matumizi ya nishati chafu ya kupikia kama kuni na mkaa.
Pongezi hizo zilitolewa katika kongamano la nishati safi na lishe, lililofanyika katika Ukumbi wa Siasa ni Kilimo, Manispaa ya Iringa ambapo Mgeni rasmi wa kongamano hilo alikuwa Mhe. Benjamin Sitta, ambaye katika hotuba yake aliweka bayana umuhimu wa kuwekeza katika teknolojia ya nishati safi kwa ajili ya afya na maendeleo endelevu ya jamii.

Mwenyekiti wa Wanawake na Samia Taifa, Fatuma Madidi amewataka wanawake kushiriki kikamilifu katika mapinduzi ya nishati safi, huku akibainisha kuwa serikali ya awamu ya sita imefungua milango ya fursa kwa wanawake kupitia sera za mazingira na nishati mbadala.
Verediana Mng’ongo ni Mwenyekiti wanawake na Samia Mkoa wa Iringa, amesema kuwa kwa kongamano hilo limewaunganisha pamoja kuhakikisha wanapata fursa ya masoko ya kuuza bidhaa zao wanazotengeneza ili kujikwamua kiuchumi.

Hata hivyo Kongamano hilo lilijikita zaidi nafasi ya kujadili nishati safi katika kuboresha lishe ya familia, kwa kuwa matumizi ya nishati salama hurahisisha maandalizi ya vyakula vyenye virutubisho bila madhara ya moshi au muda mrefu wa kupika.