Nuru FM
Nuru FM
25 August 2025, 9:39 am

Viboko walioko katika Bwawa la Mtera Wilaya ya Iringa wamekuwa kero kwa wananchi hao jambo linalohatarisha usalama wao.
Na Adelphina Kutika
Wananchi wa Kata ya Migoli, Wilaya ya Iringa, wameiomba Serikali kuchukua hatua za haraka kudhibiti wanyama wakali, hususan boko na mamba waliopo katika Bwawa la Mtera, wakidai kuwa wamekuwa chanzo cha vifo vya mara kwa mara kwa wakazi wa eneo hilo.
Ombi hilo limetolewa katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Migoli na kuongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James ,Wakazi hao wamesema wanyama hao wamekuwa tishio kwa maisha yao, hasa wanaojihusisha na shughuli za uvuvi na kuchota maji katika bwawa hilo.
Akijibu kilio cha wananchi hao, Mkuu wa Mkoa Kheri James ameagiza Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), kwa kushirikiana na mamlaka nyingine husika, kuchukua hatua za haraka ikiwa ni pamoja na kuvuna baadhi ya wanyama hao ili kuimarisha usalama wa jamii.

Kwa upande wake Mkuu wa Hifadhi Tengefu ya Lunda-mkwabi Notikelvini Mgaya amethibitisha kutokea kwa vifo vya watu wanne kati ya mwezi Julai na Agosti, vilivyotokana na kushambuliwa na boko katika eneo la bwawa hilo.
Hata hivyo Bwawa la Mtera ni chanzo muhimu cha shughuli za kiuchumi kama uvuvi, kilimo cha umwagiliaji na uzalishaji wa umeme huku likiendelea kuwa makazi ya wanyamapori hatari wakiwemo viboko na mamba, hali inayohatarisha maisha ya wananchi wanaotumia bwawa hilo.
