Nuru FM
Nuru FM
14 August 2025, 10:40 am

Elimu ya lishe iliyotolewa na Shirika la World Vision imelenga kupambana na changamoto ya lishe ambayo imeendelea kutafutiwa uvumbuzi
Na Adelphina Kutika
Wananchi wa kijiji cha Kidilo Kata ya Kihanga Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, wameendelea kuchukua hatua dhidi ya tatizo la lishe duni kwa watoto wao, kufuatia elimu inayotolewa kupitia ushirikiano kati ya serikali na shirika la World Vision ya kukabiliana na tatizo hilo.
Akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Lishe yaliyoandaliwa na Shirika la World Vision katika Shule ya Msingi Kidilo, Mkuu wa Shule hiyo Bw. Mchina Mkeng’e amesema watoto wenye udumavu hukumbwa na changamoto ya kujifunza, Jambo linaloathiri kwa kiasi kikubwa maendeleo yao ya kielimu.
Kwa upande wake, Afisa Elimu Kata Edga Madembwe amesema hali ya lishe duni imekuwa na madhara makubwa kwa wanafunzi katika kujifunza lakini kwasasa hali imebadilika baada ya serikali kwakushirikiana na shirika la world vision Tanzania kuanza kutoa elimu katika jamii juu kuhusu lishe bra kwa watoto.
Mwakilishi wa Shirika la World Vision Tanzania ambaye anasimamia mradi wa afya , lishe , usafi wa mazingira na maji kata ya kihanga Neema Temba amesema wanaendelea kutoa elimu ya ulaji bora unaozingatia makundi yote ya chakula, ili kuhakikisha watoto wanapata virutubisho vinavyohitajika kwa ukuaji wa afya na akili.
Baadhi ya wazazi wamesema elimu waliyoipata imewasaidia kubadili mtazamo kuhusu lishe na sasa wanahakikisha watoto wao wanapata chakula chenye virutubisho vya kutosha nyumbani.
Hatua hiyo inakuja wakati ambapo Iringa ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa uzalishaji wa chakula hapa nchini, lakini bado changamoto ya udumavu kwa watoto ni kubwa, hasa vijijini.
