Nuru FM
Nuru FM
19 July 2025, 9:35 am

Uzembe wa Madereva na kutofuata alama za usalama barabarani imetajwa kuwa sababu za ajali barabarani.
Na Hafidh Ally
Watu watatu wamefariki Dunia na wengine sita kujeruhiwa kufuatia ajali mbaya ya barabarani iliyotokea katika Kijiji cha Imalutwa, Kata ya Lugalo, wilayani Kilolo Mkoani Iringa.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa SACP Alan Bukumbi amesema kuwa Ajali hiyo imetokea majira ya saa 12 asubuhi katika barabara kuu ya Morogoro Iringa, ambapo gari aina ya Fuso Mini Bus lenye namba za usajili T 562 EBK, lililokuwa likiendeshwa na marehemu Akhan Mpagile (45) mkazi wa Njombe, liligonga kwa nyuma lori aina ya Howo lenye namba T857 DVZ na Trela T460 EAM mali ya kampuni ya Glenrich Transportation Co. Ltd, lililokuwa likisafiri kutoka Dar es Salaam kuelekea Iringa likiwa limebeba mzigo wa unga.

Kamanda Bukumbi ameesema kuwa ajali hiyo ilisababishwa na uzembe wa dereva wa minibus ambaye alishindwa kulimudu gari lake, hivyo kugonga kwa nyuma lori lililokuwa limesimama barabarani ambapo waliopoteza maisha ni Akhan Mpagile – dereva wa Fuso Mini Bus, mkazi wa Njombe Alfred Mgaya – utingo wa basi hilo, mkazi wa Njombe Feleschina Masigati (36) – abiria na mkazi wa Imalutwa
Kwa upande wao baadhi ya mashuhuda na manusura wa ajali hiyo wamesema kuwa walishangaa kuona abiria wakilaliana baada ya ajali kutokea huku wakiomba madereva kuweka alama barabaran pale magari yanapoharibika ili kuepusha ajali.
Watu wengine sita wamejeruhiwa na wamelazwa katika hospitali za karibu kwa ajili ya matibabu na Dereva wa lori aliyetajwa kuwa mhusika alikimbia mara baada ya ajali hiyo na juhudi za kumsaka zinaendelea.
