Nuru FM
Nuru FM
16 July 2025, 11:21 am

Mmomonyoko wa maadili kwa watoto umetajwa kuongezeka huku chanzo kikiwa ni wazazi.
Na Adelphina Kutika
Takribani watoto 1,900 mkoani Iringa wameripotiwa kukosa malezi na matunzo kutoka kwa wazazi wao, hali inayochangia kuongezeka kwa mmonyoko wa maadili katika jamii na kuathiri ustawi wa taifa kwa ujumla.
Taarifa hizo zimetolewa katika mkutano wa wazi kati ya Jeshi la Polisi na wananchi uliohusu utoaji wa elimu ya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji wa watoto, ambapo Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Iringa, Bwana Martine Chuwa, ameeleza kuwa tatizo hilo linaathiri kwa kiasi kikubwa watoto, hasa kutokana na ukosefu wa matunzo kutoka kwa baba zao.

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Faidha Suleiman amesisitiza kuwa viongozi wa dini wana jukumu kubwa la kutoa mafundisho ya kina kuhusu ndoa ili kuwawezesha wazazi kutambua majukumu yao katika malezi ya watoto.
Awali akifungua mafunzo hayo, Mgeni Rasmi ambaye ni Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto kutoka Makao Makuu ya Polisi, DCP Maria Nzuki, ameeleza kuwa lengo la utoaji wa elimu hiyo ni kupambana na ukatili wa kijinsia na udhalilishaji wa watoto ili kusaidia kurejesha maadili ndani ya jamii.
Hata hivyo Mafunzo hayo yamekuwa sehemu ya kampeni ya kitaifa ya kuelimisha jamii kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia, unyanyasaji wa watoto na umuhimu wa malezi bora kwa ustawi wa taifa.
