Nuru FM
Nuru FM
3 July 2025, 9:40 am

Katika kukabiliana na migogoro ya ardhi Wananchi 267 wamekabidhiwa hatimiliki za ardhi.
Na Mwajuma Hassan
Maboresho ya Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 toleo la 2023, yameanza kuzaa matunda kwa wananchi wa kawaida, kwa kuwezesha kurasimishwa kwa makazi, kutambua umiliki halali wa ardhi na kupunguza migogoro ya muda mrefu iliyowatesa wananchi kwa miaka mingi.
Hali hii inaonekana wazi katika Kata ya Isakalilo, Manispaa ya Iringa, ambako wananchi 267 wamekabidhiwa hatimiliki za ardhi hatua inayotajwa kama suluhisho la msingi kwa changamoto za umiliki wa ardhi.
Katika hafla ya kugawa hati hizo, iliyojaa furaha na shukrani, wakazi wa eneo hilo, wakiwemo wazee waliokuwa wakiishi kwenye ardhi hiyo kwa miongo kadhaa bila nyaraka halali, walionekana kuguswa na hatua hiyo ya kihistoria.
Mmoja wa walionufaika ni Bibi Anyesi Nyilowa, mwenye umri wa zaidi ya miaka 70, ambaye kwa mara ya kwanza baada ya miongo saba, ametambuliwa rasmi kama mmiliki halali wa ardhi anayomiliki.
Tulijua tutakufa bila kupata hati hii, lakini sasa wajukuu zetu watapata kitu cha maana katika maisha yao,” alisema kwa hisia.

Mumewe, Mzee Musa Sangwa, alikiri kuwa hapo awali hakuelewa haki ya kumiliki ardhi kwa nyaraka rasmi.
“Tulikuwa tunagawana tu na wenzetu, lakini leo nimepata hati hii,” alisema kwa furaha.
Wanandoa hawa ni mfano hai wa jinsi utekelezaji wa Sera ya Taifa ya ya Ardhi ya mwaka 1995 toleo la 2023 unavyoweza kuleta mageuzi chanya katika maisha ya watu wa kawaida kwakuondoa urasimu,Kuhakikisha usalama wa miliki pamoja na kuwezesha wananchi kiuchumi.
Devotha Kimota, mkazi mwingine wa Isakalilo aliyepokea hati yake, alieleza kuwa sasa anaweza kutumia hati hiyo kama dhamana kupata mkopo wa kuinua biashara yake.
“Nimefurahi sana kwa kuwa itanipa fursa ya kukopa katika taasisi mbalimbali za fedha,” alisema.
Kwa mujibu wa Afisa Ardhi Mteule wa Manispaa ya Iringa, Zera Chaula, zoezi hilo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa kitaifa wa kupunguza migogoro ya ardhi.
“Manispaa ya Iringa imepangiwa kuandaa hati 2,500. Hadi sasa bado hatujafikia lengo, hivyo tunahitaji kuongeza elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kurasimisha maeneo yao,” alieleza.
Hata hivyo, alibainisha kuwa uelewa mdogo kuhusu sera hiyo iliyoboreshwa bado ni changamoto, hivyo juhudi za makusudi zinahitajika kupitia vyombo vya habari na mikutano ya hadhara.
Katika kusaidia juhudi hizo, Shirika la Landesa, ambalo linajihusisha na masuala ya ardhi, limeanza kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari nchini ili kuwajengea uwezo wa kuelimisha jamii kuhusu maboresho ya sera hiyo.
“Ardhi ni hatima Kile mtakachoandika kinaweza kujenga hatima ya kizazi cha sasa na kijacho,” alisema Queen Mrema, mwakilishi wa Mkurugenzi wa Landesa Tanzania.

Masalu Luhula, mtaalamu wa Ardhi kutoka Landesa, alieleza kuwa Sera hiyo inasisitiza usawa wa kijinsia na matumizi ya njia shirikishi za amani na zenye haki katika utatuzi wa migogoro ya ardhi.
“Waandishi wa habari wana nafasi muhimu ya kuielewesha jamii kuhusu mabadiliko haya,” alisisitiza.
Naye Deodatus Mfugale, mwandishi mkongwe nchini, aliwataka wanahabari kuchambua kwa kina mabadiliko ya sera hiyo na kuwaelimisha wananchi juu ya manufaa yake.
“Waandishi wa habari waichambue sera: wajue tatizo ni nini, sera inasemaje, na wananchi watanufaikaje,” alieleza.
Kupitia maboresho haya ya sera, serikali inalenga kumaliza migogoro ya ardhi baina ya wakulima, wafugaji, wawekezaji na familia, sambamba na kuimarisha maisha ya wananchi na kukuza uchumi wa taifa kwa kuweka misingi imara ya haki ya miliki ya ardhi kwa wote.