Nuru FM
Nuru FM
2 July 2025, 2:09 pm

“Watoto yatima wanapaswa kupata msaada sawa na watoto wengine”
Na Adelphina Kutika
MBUNGE wa Jimbo la Kalenga anayemaliza muda wake Jackson Kiswaga ametoa msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo vyakula kwa Watoto yatima wanaolelewa katika kituo cha Watoto yatima Tosamaganga kilichopo katika Halmashauri ya wilaya ya Iringa.
Akizungumza mara baada ya kufika katika kituo hicho na kukabidhi msaada huo, Mbunge Kiswaga amesema kuwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za kituo hicho chenye Watoto yatima 150 kwenye jukumu la malezi ya watoto hao.
Aidha Mh. Kiswaga amewapongeza Kanisa Katoliki kwa kuwa na kituo hicho ambacho kimebeba dhamana ya kuwakusanya pamoja na kuwahudumia watoto wanaoishi katika mazingira magumu na kuwalea katika malezi bora.
Kwa upande wake Msimamizi wa Kituo hicho, Sista Hellena Kihwele, amemshukuru Mbunge Kiswaga kwa moyo wake wa kujitoa kusaidia watoto wenye uhitaji maalum, akisema kuwa msaada huo umefika wakati muafaka.
Kituo hicho cha kulea watoto yatima Tosamaganga, kwa sasa kinahudumia jumla ya watoto 150, ambapo 85 kati yao ni wakazi wa kudumu.