Nuru FM
Nuru FM
20 June 2025, 1:50 pm

Watu wenye ulemavu wanatarajiwa kunufaika na huduma za afya kwa kupata huduma za kitabibu.
Na Adelphina Kutika
Chama cha Wazazi na Walezi wa Watoto Wenye Ulemavu wa Kichwa Kikubwa na Migongo Wazi (ASBAHT) kwa mikoa ya Iringa na Njombe kimetakiwa kutoa elimu kwa jamii kuhusu shughuli zake, ili kuwasaidia watoto wenye ulemavu huo kupata matibabu na huduma stahiki.
Agizo hilo limetolewa na Afisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa wa Iringa, Bw. Martin Chuwa, ambaye alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa, wakati wa uzinduzi rasmi wa tawi la ASBAHT katika mkoa huo.
Bw. Chuwa amewataka viongozi walioteuliwa kuhakikisha kuwa wanaelimisha jamii juu ya malengo ya chama hicho ili watu wengi zaidi wajitokeze kujiunga na kusaidia watoto wenye ulemavu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa ASBAHT Taifa, Bw. Ramadhani Mwaruko, amesema hadi sasa chama hicho kimefanikiwa kufungua matawi 11 nchini kote na kimewezesha upatikanaji wa vifaa tiba katika hospitali 8 za kibingwa hapa nchini, pamoja na kuanzisha nyumba za matumaini kwa wazazi zaidi ya 150 wanaolea watoto wenye changamoto hizo.
Akiwasilisha taarifa kwa mgeni rasmi, Katibu wa ASBAHT Taifa, Bw. Said Hassan Bahari, ameomba serikali ya mkoa wa Iringa kutoa kibali kwa chama hicho kufika kwenye halmashauri za mkoa huo kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi.
Naye Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Bw. Shaaban Shomary, amewataka wazazi wanaowaficha watoto wenye ulemavu kuacha tabia hiyo, akisisitiza kuwa watoto hao wana haki ya kupata matibabu, elimu na maisha bora kama watoto wengine.
Wazazi na walezi walioshiriki uzinduzi huo wamekipongeza chama hicho kwa hatua ya kuanzisha tawi hilo, wakisema kuwa ni hatua kubwa ya kuondoa imani potofu kuwa mtoto mwenye ulemavu ni mkosi katika familia. Wamesema chama hicho kitakuwa msaada mkubwa kwa jamii kwa kutoa elimu, uhamasishaji na matumaini kwa familia zinazoishi na watoto wenye changamoto hizi.