Nuru FM
Nuru FM
19 June 2025, 11:57 am

Chama cha Mapinduzi CCM kimewaonya watia nia wa nafasi mbalimbali za uongozi kupitia chama hicho, kutotumia lugha za kebehi.
Na Godfrey Mengele
Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaotaka kutangaza nia ya kugombea nafasi za ubunge na udiwani wametakiwa kujieleza kwa hoja na kueleza sababu zinazowasukuma kugombea, badala ya kutumia majukwaa hayo kuwachafua au kuwakejeli wenzao.
Wito huo umetolewa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, MCC Salim Asas, alipokuwa akizungumza na vyombo vya Habari na kusisitiza kuwa nia ya kuwania nafasi za uongozi ni jambo la kawaida, lakini njia ya kuwasilisha dhamira hiyo lazima izingatie maadili, heshima na utaratibu wa chama.
Alisema kuwa katika kipindi hiki kutakuwa na watia nia wengi sana ambao wataita waandishi wa habari na kufanya press hiwatumie vyombo vya habari kutangaza malengo yao ya kuwania uongozi wanaotaka kwani haipendezi kwa watia nia hao kutumia fursa hiyo kuwachafua, kuwakejeli, kuwatukana na kuwashambulia wanachama wenzao.
Aliongeza kwamba Ccm kina taratibu, kanuni na miongozo ambayo kila mwanachama anapaswa kuiheshimu na endapo atashindwa kuzingatia akumbuke kuna vikao vya juu na anaweza kupepetwa kama kuchambua mchele.
Naye Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Said Goha, amesisitiza kuwa chama kitaendelea kusimamia haki, usawa na nidhamu katika mchakato mzima wa ndani ya chama.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daud Yasin, ameeleza kuwa kutangaza nia si kosa, lakini kufanya hivyo kwa kutumia lugha za matusi au kuanzisha kampeni mapema ni kinyume cha kanuni za chama.
Hata hivyo haya yanajiri kufuatia baadhi ya wanachama mbalimbali wa CCM wakianza kuonyesha nia ya kugombea nafasi mbalimbali kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.