Nuru FM
Nuru FM
3 June 2025, 11:45 am

Taasisi ya CAHE imekuwa ikisaidia na kutatua changamoto za kijamii, hasa zinazowakumba watoto
Na Ayoub Sanga
Taasisi isiyo ya kiserikali ya Caring Hearts (CAHE) imeadhimisha miaka mitatu tangu kusajiliwa kwake kwa kutembelea Kituo cha kulelea watoto yatima na wenye mahitaji maalumu cha Huruma Center kilichopo kata ya Mwangata Manispaa ya Iringa na kutoa mahitaji muhimu
Akizungumza katika tukio hilo, Mkurugenzi wa Shurika la Caring Hearts Bw. Oswald Kikoti amesema kuwa lengo kuu la taasisi hiyo ni kusaidia na kutatua changamoto za kijamii, hasa zinazowakumba watoto, vijana na wanawake.

Kwa upande wake, Mkuu wa kituo cha Huruma Center, Mchungaji Upendo Sanga ameeleza furaha yake kwao ujio wa Caring Hearts na kusema kuwa uwepo wao kituoni hapo umeleta baraka kubwa na faraja kwa watoto.
Naye mmoja wa watoto kutoka kituoni hapo Catherine Mwilapwa, kwa niaba ya watoto, ametoa shukrani kwa taasisi hiyo kwa kuwatembelea na kuonyesha upendo, akisema kuwa wamejiona wa thamani mbele ya jamii.
“Tunasema asanteni kwa kutufanya tujihisi kama familia. Mmeleta zawadi, lakini muhimu zaidi mmekuja kutuona. Tumefarijika na tunawaombea Mungu azidi kuwabariki,” amesema Catherine.
Taasisi ya Caring Hearts, iliyosajiliwa mwaka 2022, imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia makundi maalumu katika jamii, kwa kutoa misaada, elimu ya afya ya akili, uwezeshaji wa kiuchumi kwa wanawake na vijana, pamoja na kusaidia waathirika wa ukatili wa kijinsia.