Nuru FM
Nuru FM
27 May 2025, 4:03 pm

Maonesho ya Biashara na Viwanda yaliyofanyika Wilaya ya Kilolo yameonesha kuwaleta pamoja wadau mbalimbali wa sekta hizo ili kukuza soko.
Na Joyce Buganda
Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Mhe. Rebecca Nsemwa Sanga amewapongeza chemba ya biashara viwanda na Kilimo TCCIA Wilaya ya Kilolo kwa kuandaa maonesho makubwa wilayani humo kwani maonesho hayo yameitangaza Wilaya ya Kilolo kitaifa na kimataifa.
Akizungumza wakati wa kufunga maonesho hayo yaliodumu kwa siku tano kuanzia tarehe 21-25 mwezi huu katika viwanja vya Chuo cha maendeleo FDC mji mdogo wa Ilula Dc Rebecca amesema mkoa wote wa Iringa umenufaika na maonesho hayo kwani mapato yameongezeka kuanzia kipato cha mtu mmoja mmoja mpaka mapato ya kimkoa kwa ujumla.
DC Rebecca ameongeza na kusema katika maonesho hayo mzunguko wa pesa umepatikana kwa mfano wageni walilala kwenye nyumba za wageni na ilula nyumba za kulala wageni zimejaa mpaka wengine wamekwenda kulala mjini hivyo pongezi nyingi sana ziwaendee TCCIA Wilaya ya Kilolo kwa kuanzisha maonesho haya.

Kwa upande wake Katibu wa chemba ya viwanda biashara na Kilimo TCCIA Wilaya ya Kilolo Painetho Madembwe amesema lengo la maonesho hayo ni kutoa fursa kwa wakulima, wafanyabiashara na wananchi kubadilishana uzoefu.
Madembwe amesema bidhàa zenye zaidi ya Shilingi bilioni 1.5 zililetwa kiwanjani hapo kwenye mabanda yapatayo 51 hivyo mapato ya kiwilaya na kimkoa yameongezeka kwa kiasi chake.
Madembwe ameongeza na kusema maonesho hayo ni ya kwanza kufanyika hivyo wameona wapi pa kurekebisha kwa maonesho yajayo kwani kwa sasa maonesho hayo yatakuwa yanafanyika Kila mwaka pia wamependekeza kuongeza kwa muda wa Maonesho Ili kuwapa nafasi wananchi wengi kushiriki.
Kwa upande wao baadhi ya washiriki wa maonesho hayo wamesema wamefurahi kusikia maonesho hayo yatakuwa ni endelevu kutawapa Fursa Mbalimbali na muda kwa wazawa wengi zaidi kushiriki na kubainisha kuwa maonesho hayo yamepokelewa kwa upekee sana wilayani kilolo.