Nuru FM

Afisa manunuzi Kilolo akalia kuti kavu kwa kuchelewesha miradi

21 May 2025, 3:18 pm

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Peter Serukamba akiwa katika ukaguzi wa miradi ya Maendeleo Wilaya ya Kilolo. Picha na Adelphina Kutika

Kuchelewa kukamilika kwa miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Kilolo kimetajwa kusababishwa na Afisa Manunuzi ambaye alinunua Tofali moja kwa shilingi elfu 2500.

Na Adelphina Kutika

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Peter Serukamba, ametoa agizo kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, kumtafuta Afisa Manunuzi mwingine wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo baada ya aliyepo kushindwa kusimamia vizuri miradi ya maendeleo hali inayosababisha kucheleweshwa kwa utekelezaji wa miradi.

Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua ujenzi wa madarasa na mabweni katika Shule ya Sekondari ya Ifingo, Mhe.Serukamba ameonesha kukatishwa tamaa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo.

Sauti ya RC

“Shida ya miradi hii ni Afisa Manunuzi na Engeneer ,hawa ndio wanakwamisha mradi ,Katibu Tawala, naomba tutafute mbadala, Sitaki kuona hawa ndio wanamkwamisha Mkurugenzi ” amesema Serukamba

Aidha Mhe.Serukamba ametoa agizo kwamba kufikia tarehe 20 Juni 2025, mradi huo wa ujenzi uwe umekamilika bila visingizio vyovyote.

Awali, Afisa Manunuzi wa Wilaya ya Kilolo, Bi Veronica Kidua, amekiri kuwepo kwa changamoto ya kupanda kwa bei ya vifaa kutoka kwa wazabuni na umbali wa kusafirisha vifaa hivyo, jambo lililochangia kusuasua kwa mradi huo.

Sauti ya Afisa Manunuzi

Kwa upande wake Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo JOSEPH QULLA amesema  awali  tofali moja tulikuwa tunanunua kwa Shilingi 2,000, lakini sasa mzabuni anaiuza kwa Shilingi 2,500.

Sauti ya Mhandisi

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo Bi. Siwema Jumaa ameeleza wanakabiliwa na upungufu wa fedha za kukamilisha mradi huo, na kwamba tayari wameshawasilisha hoja hiyo kwa Baraza la Madiwani ili kupatiwa suluhisho.