Nuru FM
Nuru FM
18 May 2025, 8:51 pm

Mwalim Silvester aliyekosa tabasamu kwa miaka 6 baada ya kupata ajali iliyompa ulemavu ameanza safari mpya ya maisha baada ya kupatiwa kitimwendo cha umeme, miguu saidizi na toyo ya kumuingizia kipato.
Na Hafidh Ally na Fredrick Siwale
Hatimaye Mwalimu wa shule ya msingi Kinyanambo Silvester Joseph Lyuvale (57) aliyepata ajali na kukatwa miguu yote miwili amepatiwa Kitimwendo na Miguu saidizi jambo litakalosaidia kutekeleza majukumu yake.
Hatua hiyo imejiri mara baada ya Mwandishi wa Nuru FM Fredrick Siwale kuripoti uhitaji wa mwalimu huyo na Kadhia ambayo anaipata baada ya kukatwa miguu ambapo kwa muda wa miaka 6 Mwalimu huyo alikuwa akishindwa kufika shuleni kwa wakati kutekeleza majukumu yake kutokana kukosa kitimwendo kinachumia umeme jambo lililomlazimu kubonda kokoto ili aweze kupata fedha za kukodi bajaji kumpeleka shule kufundisha.
Akizungumza huku akibugujikwa na machozi ya Furaha Mwl.Silvester anayefundisha ya msingi Kinyanambo Halmashauri ya Mji Mafinga Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, amesema kuwa kupata kitimwendo hicho chenye thamani ya Milioni 12 na Miguu saidizi yenye thamani ya Milioni 10 kutoka kwa mdau wa maendeleo Mhandisi Augustino Masoyi ambaye alivyoiona taarifa hiyo akaamua kutoa msaada huo ikiwemo gharama za kumsafirisha mpaka Hospitali ya KMC kupata vifaa hivyo.
Aidha Mwalim Huyo amesema kuwa atafanya kazi kwa bidii huku akiwashukuru viongozi wa Maafisa wa Elimu Kata Wilaya ya Mufindi na Tanzania Kwa ujumla kwa kumnunulia Bajaji ya Miguu Mitatu (Toyo) ili imrahisishie kuongeza kipato yenye thamani ya shilingi Milioni 7.2 na hundi ya shilingi Milioni kumi.

Akizungumza wakati wa kukabidhi Toyo hiyo na na hundi ya shilingi milioni 10, Kaimu Mwenyekiti wa Maafisa elimu Kata Mkoa wa Iringa Mwl. Laurent Aron Mirathi amesema kuwa nguvu ya waandishi wa habari ndio imepelekea wao kupata taarifa hizo na kuamua kujichanga kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo.
“Zaidi ya halmshauri 177 zimechangia michango hiyo na kufanikiwa kupata fedha hizo na leo tunazikabidhi hapa” Alisema Kaimu Mwenyekiti

Kwa upande wake Katibu wa Chama cha kulinda na kutetea haki za walimu Tanzania (CHAKUHAWATA) Fabiani Sanga Amesema kuwa chama chao kilishiriki kwa mara nyingine tena kutoa mchango wa shilingi laki 5 kwa ajili ya kumchangia Mwl. Silvester kwa kushirikiana na Chama Cha Walimu CWT, Huku Mwakilishi wa walemavu chama cha walimu Tanzania Cresantus Euzebio Bakana akimshukuru mwanahabari wa Nuru fm Siwale kwa kuwa mstari wa mbele kufanikisha Mwalimu huyo kupata msaada huo kupitia kalamu.

Afisa Elimu Kata Kutoka Mkoa wa Kigoma Mwl Hadija Idrisa aleyesafiri kuja Mkoani Iringa kwa ajili ya kushuhudia walimu wakimkabidhi Toyo Mwl, Silvester amewapongeza waandishi wa habari kwa kufikisha changamoto iliyomkabidili Mwalim mwenzao jambo lililopelekea wachukue hatua na kumsaidia.
Bi.Christina Emmanuel Nyakunga Ni mke wa Mwalimu Silvester amewashukuru Wadau wote walioamua kumsaidia Mume wake ambaye ameondokana na adha na changamoto alizozipitia kwa miaka 6 toka akatwe miguu na kuwa mlemavu.