Nuru FM
Nuru FM
22 April 2025, 12:01 pm

Na Fredrick Siwale
Mkuu Wa Wilaya ya Mufindi Dkt. Linda Salekwa amewataka Wananchi kuwa waangalifu na kuzingatia usalama wao wanapoelekea kwenye shughuli za kujitafutia kipato, ikiwemo kuepuka kusafiri kwenye vyombo visivyokidhi vigezo vya usafiri salama.
Dkt. Salekwa ameyasema hayo wakati akiongoza mamia ya waombolezaji na wananchi wa Wilaya hiyo kuaga miili ya waliofariki kwenye ajali ya guta na gari la kubebea wagonjwa iliyotokea tarehe 19.4.2025 na kusababisha vifo vya watu 8 zoezi lililofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Upendo Mjini Mafinga.

“Guta hiyo ilikuwa imebeba watu 22, jambo ambalo si la kawaida na si salama kabisa. Watu sita walifariki dunia papo hapo, wawili walifariki dunia baadaye wakiwa hospitali akiwemo dereva wa Guta. Majeruhi wawili walipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, na wengine saba walihamishiwa Hospitali ya Ipamba,” amesema Dk. Salekwa.
Aidha, amekanusha taarifa zilizokuwa zikisambaa mitandaoni kwamba watu 15 wamepoteza maisha kwenye ajali hiyo, akisisitiza kuwa waliothibitishwa kufariki hadi sasa ni watu wanane.
“Kama mnavyoona, hapa mbele yetu tuna miili ya watu sita, na mingine miwili ilishachukuliwa na ndugu kwa taratibu nyingine. Tunawaomba wananchi wawe na utulivu na waache kusambaza taarifa zisizo sahihi,” ameongeza Dk. Salekwa.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, Cosato Chumi, ametoa pole kwa familia zilizofiwa na kupongeza jitihada za madaktari wa Hospitali ya Mji wa Mafinga kwa juhudi walizofanya kuwaokoa majeruhi wa ajali hiyo.
“Nawashukuru pia wananchi wa Mafinga kwa namna walivyojitokeza kusaidia kwa hali na mali baada ya ajali hiyo kutokea, ikiwemo kutoa misaada ya haraka kwa majeruhi,” amesema Chumi.
Awali Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mufindi, George Kavenuke, ameiomba Serikali kupitia vyombo vya usalama barabarani kuendelea kutoa elimu na maelekezo kwa madereva wa vyombo vya moto juu ya kuzingatia sheria za usalama barabarani.

Ajali hiyo ilitokea Aprili 19, 2025 saa 12:30 asubuhi, katika eneo la Luganga, barabara ya Mafinga-Mgololo na kusababisha vifo vya watu nane, akiwemo dereva wa Guta, huku wengine 14 wakijeruhiwa ambapo walioagwa ni Latifa Joseph Ngela (18), Irene Msanga (55), Siamini Lukosi, Rukia Kasavaga (52), Jenipha Msigwa (42), Anord Mbosso. Jema Mbwilo (50) na Adofu Ndanzi (27), ambapo miili yao ilichukuliwa na ndugu kwa taratibu za mazishi ya kifamilia nyumbani.