Nuru FM

TLS Kanda ya Iringa yapata viongozi wapya, Wakili Ambindwile atetea kiti chake

17 April 2025, 6:48 pm

Viongozi wa TLS Taifa, Kanda ya Iringa na Jaji Mfawidhi wakiwa katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa TLS Iringa. Picha na Hafidh Ally

Na Hafidh Ally

Wakili Moses Ambindwile amefanikiwa kutetea nafasi ya Mwenyekiti wa Chama cha wanasheria Tanganyika TLS Kanda ya Iringa kwa kupata Kura zote 45 katika uchaguzi uliofanyika leo Kwenye ukumbi wa siasa ni kilimo Manispaa ya Iringa.

Katika Uchaguzi huo Uliofanyika sambamba na zoezi la Mkutano mkuu maalumu wa mwaka wa TLS Kanda ya Iringa, Wakili Ambindwile alikuwa mgombea pekee wa nafasi ya mwenyekiti huku nafasi nyingine zikiwa na wagombea mbalimbali.

Kwenye nafasi ya Makamu mwenyekiti kulikuwa na wagombea watatu ambapo Jessey Mwamgiga ameshinda nafasi hiyo kwa kupata kura 19, akiwabwaga Wakili Emanuel Chengula aliyepata kura 16 na Wakili Vedasto Chonya aliyepata kura 10 katika kinyang’anyiro hicho.

Wakili Moses Mwenyekiti wa TLS Iringa

Akizungumza wakati wa Mkutano huo, Mgeni Rasmi Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu  Tanzania Kanda ya Iringa Mh. Dunstan Ndunguru amewataka viongozi wapya kuhakikisha wanasimamia haki na kuimarisha utawala bora katika jamii.

“TLS mna jukumu la kuhakikisha mnasimamia Haki na kuimarisha utawala bora hapa Nchini kupitia Kifungu cha tatu cha TLS kinachoagiza kufanya hivyo pamoja na kujadili maendeleo ya  chama” Alisema Jaji Ndunguru

Moses Ambindwile ni Mwenyekiti wa TLS Kanda ya Iringa amesema kuwa kwa sasa wana jukumu la kuhakikisha wananchi ambao wanashindwa kumudu gharama za kuwalipa mawakili kusimamia kesi zao wanawapa kipaumbele kwa kuangalia vigezo ambavyo wameviweka.

Sauti ya Rais Ambindwile

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Chama cha wanasheria Tanganyika TLS Leticia Petro Ntagazwa amesema kuwa ni vyema mawakili wakaheshimiwa kama watendaji wengine wa mahakama na ikiwezekana wakaboreshewa maslahi yao.

“Tuna changamoto pia katika sheria za Mawakili kumfanya Jaji au Hakimu wa Mahakama kumsimamisha wakili akiwa anatekeleza majukumu yake kitu ambacho kinawafanya mawakili kuwa wanyonge wakati wa kuwatetea wateja wao, Na wakati mwingine wakili wa serikali wanathaminiwa hata wakichelewa kwenye kesi hawafokewi wala  kuonywa kama Mawakili wa kujitegemea” Alisema Makamu wa TLS

Sauti ya Makamu Rais TLS

Uchaguzi huo ulihudhuriwa na wadau mbalimbali wa haki jinai wakiwemo maofisa wa TAKUKURU, Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Mahakimu wa Mahakama ya Mwanzo na Mahakama Kuu, pamoja na wawakilishi kutoka ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa (RCO).