

3 March 2025, 11:09 am
Na Fredrick Siwale
TUME ya haki za binadamu na Utawala bora Nchini imetoa mafunzo kwa Watendaji wa Vijiji na Mitaa, wa Halmashauri ya Mafinga Mji na Wilaya ya Mufindi kuhusu haki na Wajibu kwa Wananchi.
Akizungumza wakati wa Mafunzo hayo, Kamishna wa tume ya haki za binadamu na Utawala bora Nchini Dkt.Thomas Masanja ,amesema Watendaji hao wanapaswa kuzingatia kanuni, taratibu na Sheria katika utekelezaji wa majukumu yao badala ya kujiamlia wanavyotaka.
Bi.Fides Shao kutoka Tume ya haki za binadamu na Utawala bora,aliwataka Watendaji hao kuhakikisha kuwa eneo lolote ambalo Mwananchi atakuwa anashikiliwa kwa mjibu wa Sheria vigezo na haki za mhusika zinapaswa kulindwa na kwa kuzingatia miongozo.
Naye Afisa Uchunguzi Mkuu na Mratibu wa Jinsia na haki za Watoto kutoka Tume hiyo Bi. Florence Chaki amewataka Maafisa Watendaji hao kutoa taarifa za mapato na matumizi kwa Wananchi kwa misingi ya Utawala wa kisheria na kuzingatia haki za binadamu.
Kwa Upande wake Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Ivambinungu Bi. Imara Mbena ameushukuru Uongozi wa Halmashauri ya Mji Mafinga na Viongozi wa tume kwa kuwapa mafunzo hayo ambayo yatawasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao.
MWISHO