

19 February 2025, 12:24 pm
Na Adelphina Kutika
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora Nchini inatarajia kutoa elimu kuhusu misingi ya haki na Utawala bora kwa wananchi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Iringa kwa lengo la kuwawezesha Wananchi kutambua haki zao na kudumisha Utawala unaozingatia haki za binadamu.
Hayo yamebainishwa na Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora Dkt. Thobias Masanja wakati Akizungumza na Vyombo vya Habari katika ofisi ya Mkoa wa Iringa kuhusu zoezi la kutoa elimu kwa wananchi katika Halmashauri mbalimbali za Mkoa wa Iringa.
Masanja ameeleza kuwa mikutano hiyo itatumika kuitambulisha Tume kwa wananchi, kuwaskiliza na kupokea malalamiko yao yanayohusu haki za binadamu na utawala bora katika maeneo yao.
Aidha, Dkt. Masanja amesema kuwa elimu ya misingi ya haki za binadamu na utawala bora itatolewa kwa wanafunzi katika shule za sekondari na vyuo mbalimbali, ili kuwajengea uelewa na kuwaandaa kwa mustakabali wa kuwa viongozi bora katika siku zijazo.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Iringa Press clabu Frank Leonard ameipongeza tume hiyo kwa kufika mkoani Iringa kuja kitoa elimu kwa jamii juu misimgi ya utawala bora pamoja na kutambua haki zao.
Aidha, zoezi hilo litaambatana na kutembelea Magereza za Mkoa hapa kwa lengo kukagua na kutathmini haki za watu wanaozuiliwa, na kutoa mapendekezo jinsi ya kutatua matatizo yaliyopo kwa mujibu wa taratibu na Sheria zilizopo ikiwa ni pamoja na kukagua viwango vya kimataifa na kikanda vinavyolinda na kutetea haki za binadamu ikiwemo makundi ya watu waliozuiliwa.
MWISHO