

17 February 2025, 10:15 am
Na Fredrick Siwale
Wananchi wa Mtaa wa Ihongole uliopo kata ya Boma Halmashauri ya Mji Mafinga wameiomba serikali iwajengee daraja linalotumiwa na wanafunzi kuelekea shule ya JJ na Nyamalala ili kuwanusuru na hatari ya kusombwa na maji ya mvua.
Wakizungumza na Nuru FM baadhi ya wananchi wa mtaa huo wamesema kuwa wamekuwa wakiwavusha watoto wao kwenda upande wa pili wa mtaa wa Ivambinungu kutokana na daraja lililopo kutokuwa katika ubora.
Aidha wamesema kuwa ni vyema serikali ikachukua tahadhari kwani wakati wa mvua miongoni mwao wamekuwa wakipoteza mali zao huku wakihatarisha maisha yao pindi wakipita katika daraja hilo.
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Ihongole Pasto Atanas Madenge amesema kuwa walishirikiana na diwani kuweka magogo katika daraja hilo huku akiiomba Halmashauri kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wake.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Boma Mh.Julist Kisoma anawaondoa hofu Wananchi kwa kueleza kuwa ujenzi wa daraja hilo upo kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 na litatekelezwa na Tarura Wilaya ya Mufindi.
MWISHO