Madereva Iringa waaswa kuongeza umakini barabarani
19 December 2024, 9:09 am
Na Zahara Said na Halima Abdallah
Kuelekea sikukuu za Mwisho wa Mwaka, Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Iringa limewataka madereva kuwa makini pindi wanapoendesha vyombo vya moto ili kupunguza ajali barabarani.
Hayo yamezungumwa na Mtahini wa Madereva Mkoani Iringa Sajenti Hassani na kuongeza kuwa madereva wanapaswa kuongeza umakini sambamba na kukagua magari yao ili kujiridhisha kama ni salama kabla ya kuanza safari.
Sajent Hassani amewataka wamiliki wa vyombo vya moto kupeleka vyombo kwa ajili ya ukaguzi bila malipo yoyote ili kuvifanyia matengenezo vyombo hivyo kabla ya kuanza safari hasa za masafa marefu.
Hata hivyo wananchi Manispaa ya Iringa wamewashauri madereva kufuata sheria za barabarani na kupeleka vyombo vikakaguliwe ili kuepusha ajali katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka.
Katika kuhakikisha usalama unaendelea kuwepo barabarani Jeshi la Polisi Mkoani iringa linafanya operesheni kali kwa vyombo vya moto, madereva pamoja na kutoa elimu kwa madereva kuhusu usalama barabarani.
MWISHO