Mwili wa mchungaji aliyedai akifa atafufuka wazikwa mkoani Iringa
7 December 2024, 10:40 am
Na Mwandishi wetu
Mchungaji wa Kanisa la El-Huruma (E.H.C), John Chida, ambaye mwili wake ulihifadhiwa ndani ya nyumba kwa miezi miwili tangu alipofariki dunia ikisubiriwa kuwa angefufuka, umezikwa.
Mwili wa Chida (47), umezikwa katika makaburi ya Mlolo, Manispaa ya Iringa baada ya ndugu zake kupata taarifa kupitia vyombo vya habari ndugu kufariki dunia Oktoba, 2024 uligunduliwa Desemba 3, ndani ya nyumba yake ukiwa umeharibika.
Muumini wa kanisa hilo, Agnes Mwakijale, anashikiliwa na polisi mkoani Iringa ikidaiwa alikuwa akiishi ndani na mwili wa mchungaji huyo akiamini angefufuka.
Ibada ya mazishi ya Chida imeongozwa na Mchungaji Godfrey Hezron wa Kanisa la ACTS Fellowship ambaye amesema hawawezi kufumbia macho matukio kama hayo.
Ruti Chida, mtoto wa marehemu amesema alipata taarifa kuhusu tukio hilo kupitia kwa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Isakalilo C, Amos Msole, kuwa baba yake amefariki tangu Oktoba.
“Taarifa ya msiba tumeipata kupitia vyombo vya habari, tumefika usiku kwa ajili ya kumpumzisha ndugu yetu katika makaburi ya Mlolo,” amesema.
Ameishukuru Serikali kupitia mwenyekiti wa kitongoji cha Isakalilo ‘C’ na Jeshi la Polisi kwa kuwa nao bega kwa bega katika msiba huo.
Chida alizaliwa mwaka 1977 mjini Kongwa mkoani Dodoma.