Water for Africa lachimba kisima shule ya Mjimwema, wazazi kuchangia elfu 7
23 October 2024, 10:51 am
Na Fredrick Siwale
Wananchi wa Kata ya Boma Halmashauri ya Mji Mafinga Mkoani Iringa wameridhia kuchanga fedha kiasi cha shilingi elfu 7 kila mzazi ili zisaide kujenga miundombinu ya maji katika mradi wa kisima uliojengwa shule ya Msingi Mji Mwema.
Akizungumza katika hafla fupi ya kuchangia Ujenzi wa miundo mbinu ya maji katika Shule hiyo Mwenyekiti wa kamati ya Shule Bw.Roges Mselu amewaomba Wazazi kila mmoja kuchangia shilingi elfu saba kwa idadi ya Wanafunzi 800 waliopo ili zipatikane fedha za ujenzi wa miundombinu ya maji baada ya Shirika la Water For Afrika kuwachimbia kisima.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mjimwema Mwl. Ireen Makanja amesema kuwa makadirio ya fedha zinazotakiwa kuchangia ukamilishaji wa Ujenzi wa miundo mbinu ya maji ni shilingi 5.5 milioni.
Awali Diwani wa Kata ya Boma Halmashauri ya Mji Mafinga Mhe Justis Kisoma amelishukuru shirika la Water For Afrika kwa kuwachimbia kisima na kufunga Pampu katika shule ya Msingi Mjimwema huku akiwataka wananchi kutunza miundombinu baada ya kukamilika.
Nao wazazi wa wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo wameridhia kutoa fedha hizo huku wakiomba wanafunzi ambao ni yatima wasiwekwe katika orodha ya kuchangia ili wao waongezee fedha zilizosalia.
MWISHO