Wanaoingiza mifugo hifadhi ya taifa Ruaha waonywa
23 October 2024, 9:38 am
Na Hafidh Ally
Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), limeonya baadhi ya watu wanaowapotosha wafugaji wilayani Mbarali katika Mkoa wa Mbeya kwamba Serikali imeruhusu kuingiza mifugo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha likidai kuwa taarifa hizo sio za kweli na litachukua hatua.
Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Godwell Ole Ming’ataki ameyasema hayo alipozungumza na wandishi wa habari kuhusu tatizo la makundi ya mifugo kuingizwa ndani ya hifadhi hiyo katika kipindi hiki cha ukame.
Amesema wakiikamata mifugo hiyo wataendelea kuwachukulia hatua kali za kisheria ikiwemo kuwapeleka mahakamani na kuitaifisha hali ambayo itawasababishia hasara wafugaji hao.
Naye Katibu wa wafugaji Wilaya ya Mbarali Bariki Julias amewasihi wafugaji wenzake kujua umuhimu wa hifadhi ya Taifa ya Ruaha kwani husaidia kukuza uchumi wa nchini.
Amesema wanaendelea kutoa elimu kwa wafugaji katika maeneo mbalimbali wilayani humo ili waelewe umuhimu wa hifadhi hiyo na kuacha kuingiza mifugo.
MWISHO