Bilioni 142 kujenga barabara ya Iringa kwenda hifadhi ya Taifa ya Ruaha
24 September 2024, 9:46 am
Na Godfrey Mengele
Serikali kupitia Wakala ya Barabara (TANROADS) imesaini mkataba wa ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya Iringa – Msembe yenye urefu wa kilometa 104 inayoelekea kwenye Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ikijengwa na mkandarasi (CHICO Limited).
Hafla ya kusaini Mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo ambao utagharimu Shilingi bilioni 142.56 umesainiwa katika uwanja wa Samora mkoani Iringa mbele ya Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa, wananchi, viongozi mbalimbali wa dini na serikali huku.
Kwa mujibu wa Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa amesema kuwa serikali inatambua umuhimu wa ujenzi wake kwani kukamilika kwake kutakuwa na manufaa kwa wananchi na kufungua fursa za kiutalii, kiuchumi na kibiashara kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Isimani na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi amesema kwa kipindi cha miaka 30 ya ubunge wake na wabunge wengine wamekuwa wakifuatilia juu ya ujenzi wa barabara hiyo pasina mafanikio hadi sasa kuanza kwa mchakato huu na kumshuruku Rais Dk samia kutoa fedha.
Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mohamed Besta amesema kuwa mkataba huo unatekelezwa kwa miezi 24 na kumtaka mkandarasi kutekeleza kazi hiyo kwa mujibu wa mkataba na kukamilisha kwa wakati.
MWISHO