Wenyeviti wa vijiji waaswa kusimamia miradi ya maendeleo
30 August 2024, 10:27 am
Na Adelphina Kutika na Ayoub Sanga
Wenyeviti wa Serikali ya Vijiji katika Halmashauri za Iringa wametakiwa kusimamia miradi ya Wadau wa Maendeleo inayolenga vijana ili kuhakikisha utekelezaji wake unafanyika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Wito huo umetolewa na Afisa Maendeleo Mkoa wa Iringa, Bi. Saida, ambaye alikuwa mgeni katika kikao kilichoandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Lyra in Africa Cha Kutambulisha mradi wa Ujuzi wa Kujiajiri kwa vijana chini ya ufadhili wa SWISSCONTACT, Saida ametoa maelekezo kwa viongozi kuhusu namna bora ya kuwasimamia vijana kufanya kazi.
Aidha, Bi. Saida amelipongeza Shirika la Lyra in Africa kwa jitihada zao za kuwajengea vijana stadi za maisha inayolenga kuwajengea uwezo wa kujitambua.
Gift Mafue, mratibu wa mradi kutoka shirika la Lyra, amesema kuwa lengo la mradi huu ni kutoa mafunzo kwa vijana wapatao 150 wenye umri wa miaka 15 hadi 25, ambao wako nje ya shule, ili waweze kupata ujuzi wa kujiajiri na kukuza vipato vyao.
Naye Meneja wa Miradi wa shirika la lyra in Africa Nora Mkenda amesema vijana watakaochaguliwa lazima wawe na uwezo wa Kutumia ujuzi watakaopata Kwa vitendo na kuhamishia kwenye jamii zao.
Hata hivyo shirika la Lyra in Africa limejikita katika maeneo makuu manne ya utekelezaji wa miradi: ujenzi wa mabweni ya wasichana katika shule za sekondari vijijini, kuweka maabara za kompyuta, na kutoa ufadhili kwa wanafunzi wanaoishi katika mazingira magumu.
MWISHO