CAMFED kuja na filamu kuhamasisha elimu kwa mtoto wa kike
26 August 2024, 10:06 am
Elimu ya watoto wa kike ni moja ya njia bora za kupunguza umaskini, mimba na ndoa za utotoni katika mataifa yanayostawi.
Na Adelphina Kutika
Wadau wa elimu mkoani Iringa wamelitaka shirika la Campaign for Female Education (CAMFED) kuisambaza kwenye jamii na maeneo ya shule za bweni filamu ya “Tunainuana” iliyoandaliwa na mwazilishi wa mtandao wa Wasichana Wasomi wa Africa hapa nchini Bi Lydia Wilbard ili kuleta mabadiliko chanya katika kumuelimisha mtoto wa kike.
Akizungumza mara baada ya hafla ya kutizama filamu hiyo, Afisa Vijana wa halmashauri ya wilaya ya Iringa Bw. Hamis Sabuni amesema filamu hiyo ikipelekwa kwenye jamii itabadilisha mitizamo ya wazee vijijini wanaoamini mtoto wa kike hapaswi kupata elimu.
Mratibu wa CAMFED Wilaya ya Iringa Vijijini Maua Omary, amesema kuwa lengo la kuonesha filamu hiyo ni kuonyesha jinsi mtoto wa kike anavyoweza kushinda changamoto zinazomkabili na kufikia malengo yake.
Winnie Oscar Boaz, mmoja wa wananchi walioshiriki hafla hiyo, amesema kwamba amejifunza kuwa mtoto wa kike akiwezeshwa kielimu anaweza kujitambua na kutimiza ndoto zake.
Baadhi ya wanaCAMA waliohudhuria hafla hiyo wameeleza kuwa filamu hiyo imewafundisha namna ya kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kumuelimisha mtoto wa kike
MWISHO