Wakazi wa Jimbo la Isimani waagizwa kujiandikisha daftari la mpiga kura
13 August 2024, 10:13 am
Na Adelphina Kutika
Wakazi wa kata ya Malengamakali, Jimbo la Isimani, wilaya ya Iringa, wametakiwa kujiandikisha katika daftari la mpiga kura ili waweze kushiriki zoezi la uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi Mkuu mwakani.
Wito huo umetolewa na Afisa Tarafa wa Jimbo la Isimani, Thomas Myinga, wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Iguluba na Usolanga ambapo ameeleza kuwa wanaopaswa kujiandikisha ni wale wenye umri wa miaka 17 na waliohama makazi.
Kwa upande wao makatibu wa Jimbo la Isimani ,Israel Chotamasege na Amos Ndaso , wamesema wananchi wanatakiwa kuboresha taarifa zao kwenye daftari la mpiga kura ili kupata nafasi ya kupiga kura na kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.
Mwenyekiti wa kijiji Cha Iguluba benitho Garus Mkisi amewataka vijana kuhakikisha wanadumisha upendo na amani kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unahusisha kuchagua viongozi kwenye nafasi za Mwenyekiti wa Kijiji, Mwenyekiti wa Kitongoji, Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji (Mchanganyiko) na Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji (Kundi la Wanawake).
MWISHO