Mkazi wa Saadan akuta msalaba mlangoni kwake
7 July 2024, 10:50 am
Vitendo vya kutishiana maisha vimeshamiri katika kijiji cha Saadan mkoani Iringa baada ya kijana wa kijiji hicho kuamka asubuhi na kukuta msalaba wa mtu aliyefariki dunia toka mwaka 1997.
Na Hafidh Ally na Azory Orema
Mkazi wa kijiji cha Saadani kata ya Masaka mkoani Iringa Anderson Mhela amepatwa na mshtuko baada ya kuamka asubuhi na kukuta msalaba ukiwa mlango kwake.
Akizungumzia mkasa huo Mhela amesema kuwa amekutana na msalaba Ulioandikwa Jina la Marehemu Boni Nyambeke aliyefarriki dunia mwaka 1997 ambapo alitoa taarifa kwa uongozi wa kijiji kwa hatua zaidi huku akibainisha kuwa hizo ni hujuma za vijana dhidi yake.
Nao baadhi ya wananchi wa kijiji cha Saadan wamesema kuwa kijiji chao kimekuwa na matukio ya ajabu katika kijiji hicho ikiwemo kuchomewa nyumba, kuwekewa misalaba na kutishiwa maisha huku mwenyekiti wa kijiji Bastin Chengula akikiri kuwepo kwa tukio hilo na hatua wameanza kuchukua kubaini wahusika.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Masaka Mh. Methew Nganyagwa amesema kuwa ataitisha mkutano wa kijiji na kujadili kuhusu vitisho dhidi ya Raia wa eneo hilo.
Nuru FM tulimtafuta Mkuu wa Wilaya ya Iringa Kheri James kuzungumzia changamoto hizo na kuahidi kuwafikia wananchi hao ili waweze kujadili namna ya kukabiliana nazo.