Nuru FM

Tozo ya majengo kupitia manunuzi ya Umeme kilio kwa wanairinga

4 July 2024, 11:16 am

Wananchi wamelalamika kuongezeka makato ya kodi ya majengo kuanzia Julai Mosi 2024.

Na Michael Mundellah na Naida Atannas

Wananchi Manispa ya Iringa wamelalamikia kuona ongezeko la tozo ya makato ya kodi ya majengo kuanzia Julai Mosi 2024 pindi wanaponunua umeme kutoka shilingi 1500 mpaka shilingi 2000.

Wakizungumza na Nuru fm baadhi ya wananchi hao wamesema kuwa mabadiliko ya tozo hizo yanazidi kuwakandamiza wananchi wenye kipato cha chini.

Sauti ya Wananchi

Aidha wananchi hao wameiomba serikali kuwapunguzia gharama za tozo pindi wanaponunua umeme ili waweze kuzimudu.

Sauti ya wananchi

Shirika la Umeme Tanzania Tanesco kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano na Mahusiano kwa Umma limesema ongezeko hilo ni malipo ya deni walilopaswa kukatwa Julai, 2023 ambapo mteja ataendelea kulipia viwango vya kawaida kulingana na aina ya nyumba anayoishi baada ya kukatwa fedha hizo mwezi huu.

“Tunapenda kuufahamisha umma kwamba, hakuna ongezeko lolote lililofanyika kwenye viwango vya kodi ya majengo nchini isipokuwa ni madeni ya nyuma yaliyotakiwa kulipwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024,” imeeleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa Tanesco, baada ya mabadiliko ya kodi hiyo yaliyotangazwa Julai 26, 2023 kutoka Sh1,000 hadi Sh1,500 kwa nyumba za kawaida na Sh5,000 hadi Sh7,500 kwa nyumba za ghorofa, ilimaanisha mteja aliyenunua umeme kati ya Julai Mosi hadi 25, mwaka jana (kabla ya mabadiliko ya viwango vya kodi kuanza) alilipa kiwango cha zamani, yaani Sh1,000 na hivyo kuwa na baki ya deni la Sh500 ambayo alitakiwa kulipa.

Tanesco imesema kwa kuwa madeni ya fedha hizo hayakulipwa kwa baadhi ya wateja, kinachotokea sasa ambao ni mwaka mpya wa fedha 2024/25 ni kwa mteja kukatwa kiwango ambacho hakikulipwa.

“Makato ya madeni hayo yatafanyika kwa mara moja tu na yanatakiwa kulipwa kwa pamoja wakati mteja akifanya manunuzi ya umeme kwa mara ya kwanza kuanzia Julai 2024,” imeeleza.

Shirika hilo limesema baada ya Julai, mteja ataendelea kulipia viwango vya kawaida kulingana na aina ya nyumba anayoishi.

MWISHO