Wananchi Iringa waomba serikali kuingilia kati mgogoro wa ardhi
5 June 2024, 12:22 pm
Migogoro ya ardhi imetajwa kuwa sababu ya Wananchi Wilaya ya Iringa kutokuwa na maelewano.
Na Adelphina Kutika
Wananchi wa Tarafa za Idodi na Tarafa ya Kiponzero iliyopo ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Iringa wameiomba Serikali kutatua changamoto ya Mgogoro wa ardhi inayopelekea wananchi kupigana.
Hayo yamezungumzwa na Wenyeviti wa vijiji vya Tarafa hizo na kuongeza kuwa wakulima walivamiwa na wananchi wa idodi hali inayosababisha kuharibu mazao ya wakulima huku wakiiomba serikali kuingilia kati.
Awali Diwani wa Kata ya Kihanga Khamis Sabuni Nziku amesema toka alivyoingia madarakani changamoto inayowakabili ni mgogoro wa ardhi hali inayopelekea wananchi kutokuwa na maelewano.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Iringa Kheri James amewaagiza wataalamu wa ardhi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Vijijini kushughulikia kero ya ardhi katika tarafa ya Idodi na Tarafa ya Kiponzero iliyopo ndani ya Halmashauri hiyo na kupeleka mrejesho ndani ya siku saba.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Wilaya ameagiza wataalamu kuwa na utaratibu wa kukagua miradi ya maendeleo pamoja na kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili wananchi wa Kata ya Kihanga,Wasa na Maboga zilizopo katika Halmashauri hiyo.
MWISHO