Serikali yasikitika TRAMPA na TAPSEA kutoshiriki kikao kazi
10 May 2024, 12:32 pm
Waajiri wanaoshindwa kuwapa Fursa ya kupata mafunzo waajiriwa wao waonywa ili kuongeza uelewa kwa watendaji hao.
Na Adelphina Kutika
Serikali imechukizwa na kitendo cha baadhi ya Waajiri wa Taasisi za Umma kwa kutowaruhusu na kuwagharamia Wanachama wa Chama cha Taaluma ya Menejimenti ya kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) na Wanachama wa Chama Cha Makatibu Muhsusi (TAPSEA) kushiriki kikao kazi.
Hayo yamezungumzwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene, wakati akifunga mafunzo ya uadilifu na utunzaji siri kwa watunza kumbukumbu na nyaraka na makatibu mahsusi kutoka Tanzania bara na Zanzibar kwenye mkutano uliofanyika Mkoani Iringa na kusema kuwa waajiri waliokiuka maagizo ya Rais hatua zitachukuliwa dhidi yao.
Akiwasilisha taarifa mbele ya Waziri Simbachawene, Mwenyekiti wa TRAMPA, Devotha Mrope amesema wanakabiliwa na changamoto ya baadhi ya waajiri kutokupokea vyema mafunzo hayo na kuwazuia wataalamu kutoshiriki kikao kazi hicho.
Gwamaka Endrew Ngomale Makamu Mwenyekiti TRAMPA Taifa amesema mafunzo hayo yamekuwa chachu kwa watunza kumbukumbu, kwani yatasaidia kutunza siri za serikali.
Aidha Mafunzo ya Wanachama wa Chama cha Taaluma ya Menejimenti ya kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) na Wanachama wa Chama Cha Makatibu Muhsusi (TAPSEA) M yalianza may 6 2024 mpaka may 9 2024 yakiwa na washiriki wapatao 1500 kutoka Tanzania bara na visiwani Zanzibar
MWISHO