Prof. Mkenda: Mvua ikinyesha kubwa usiruhusu mtoto aende shule
25 April 2024, 10:22 am
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitangaza mwendelezo wa mvua katika mikoa mbalimbali nchini na kuwataka wananchi kuchukua tahadhari huku Wizara ya elimu ikitoa tahadhari kwa wazazi juu ya usalama wa watoto wao.
Na mwandishi wetu
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amewataka wazazi na walezi wasiwaruhusu watoto kwenda shule mvua ikiwa inanyesha kubwa.
Prof. Mkenda amesema mvua kubwa zinazoendelea kunyesha ni vyema wazazi wakachukua tahadhari kuepusha majanga.
“Mzazi ukiona mvua ni kubwa usimruhusu mtoto wako aende shule, akikosa siku moja au mbili si vibaya, tunazipongeza shule ambazo zimeshachukua hatua za kusitisha masomo kipindi hiki,” amesema.
Hatua hiyo inatokana na mvua kubwa zinazonyesha na kusababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara kupitika kwa shida pamoja na baadhi ya shule kuzingirwa na maji.
Jumanne, Aprili 23, 2024, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitangaza mwendelezo wa mvua katika mikoa mbalimbali nchini na kuwataka wananchi kuchukua tahadhari.
Mvua hizo ndizo zilizosababisha vifo vya wanafunzi saba wa Shule ya Msingi Ghati Memorial iliyopo Murieti jijini Arusha baada ya gari la shule kusombwa na maji Aprili 12, 2024.
“Wazazi hasa wa shule binafsi ndio wanakomaa watoto waende shule kipindi hiki cha mvua na wengi wa watoto wanasoma mbali na mazingira wanayoishi, tumeshuhudia magari yanakwama barabarani kutokana na barabara kujaa maji, mtoto akikosa shule kwa kipindi hiki si vibaya, serikali itaangalia namna ya kufidia, ”amesema Prof. Mkenda na kuongeza:
“Kuna tathmini inafanyika ya shule zote za Tanzania Bara zilizoathirika, Kamishna wa Elimu atakuja na tamko rasmi, tunaweza kufidia siku ambazo watoto watapoteza masomo, ”amesema.
Ameagiza shule zote za umma na binafsi kuwapokea watoto ambao shule zao zimekumbwa na mafuriko kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
“Familia zimehama, naagiza huko walikoenda shule zilizopo karibuni ziwapokee watoto waendelee na masomo bila masharti yoyote, kama kuna taratibu nyingine zitafuata baadaye,”amesema Mkenda na kuongeza
“Agizo hili si kwa shule za umma peke yake hata zile za binafsi, kuna shule za binafsi zimeathirika, hivyo mzazi anaweza kumpeleka mtoto kwenye shule nyingine ya binafsi anayohitaji bila masharti yoyote na kama kuna msaada wowote watahitaji kutoka serikalini tupo tayari kusaidia, tayari nimeshatoa maagizo kwa Kamishna wa Elimu,” amesema.