Waonywa kuacha kuwatumikisha watoto katika uchungaji wa mifugo
24 April 2024, 10:27 am
Licha ya serikali kuweka mazingira rafiki kwa watoto kusoma bado kuna baadhi ya wazazi wamekuwa na tabia ya kuwapeleka watoto kuchunga mifugo.
Na Joyce Buganda
Jamii ya wafugaji Kata ya Kiwele Halmashauri ya Wilaya ya Iringa imetakiwa kuwapeleka watoto wao shule badala ya kuwatumikisha katika kazi za kuchunga mifugo.
Akizungumza katika kikao cha wafugaji Diwani wa kata hiyo Felix Waya kilichoketi kwa ajili ya uchaguzi wa viongozi amesema kuwa kutakuwa na operesheni ya kuwasaka watoto wenye umri wa kuanza darasa la kwanza lakini wanafanyishwa shughuli za uchungaji na walioolewa mara baada ya kuhitimu darasa la saba ili wapate haki yao ya elimu.
Naye Afisa Maendeleo kata ya Kiwele Magdalena Mkwawi amesema kuna baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwaambia watoto wao wafanye vibaya katika mitihani yao ya darasa la saba ili wafeli kisha waolewe.
Kwa upande wao wananchi wamesema kuwa hali hiyo imepungua tofauti na awali na wameeleza sababu ni wazazi kuwakatisha tamaa watoto kwa sababu ya uchumi ni mgumu.
MWISHO