Wagombea Chadema Iringa warudisha fomu
3 April 2024, 9:23 am
Uchaguzi wa Chadema una lenga kupata Viongozi wapya watakaokiongoza Chama hicho baada ya walioko madarakani kumaliza muda wake kwa mujibu wa katiba Yao.
Na Godfrey Mengele
Viongozi wanaogombea nafasi mbalimbali ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema Mkoani wa Iringa wamerudisha fomu za kugombea nafasi hizo huku wakibeba ajenda za kupambana na tatizo la afya na ajira.
Wakizungumza wakati wa zoezi la urejeshaji wa fomu hizo Mgombea nafasi ya Mwenyekiti Baraza la Wazee Bw Elikus Ngweta pamoja na Suzan Mgonokulima Mgombea nafasi Mwenyekiti Baraza la Wanawake wamesema utoaji huduma ya afya umekuwa si wakuridhisha kuliko yanayozungumzwa katika majukwaa ya kisiasa.
Vitusi Nkuna Mgombea nafasi ya Mwenyekiti Baraza la vijana Chadema Mkoa wa Iringa amesema anagombea nafasi hiyo kwani baraza hilo limekusudia katika chaguzi za mwaka huu 2024 na ule wa mwakani 2025 kupata wagombea vijana kushika nafasi hizo ili kutetea makundi mengine.
Kwa upande wake William Mungai Mwenyekiti wa chadema Mkoa wa Iringa anae gombea tena nafasi hiyo amesema kuwa anagombea tena nafasi hiyo ili kukamilisha yaliyoanzishwa na wagombea wenzake ikiwamo suala la ujenzi wa ofisi ya chama hicho.
Uchaguzi ndani ya chama cha demokrasia na maendeleo chadema unatarajiwa kufanyika tarehe 9/4/2024 ili kupata safu ya uongozi watakao ongoza chama hicho kwa kipindi cha miaka mitano.