Mafinga mji kunufaika na mradi wa TACTIC
26 March 2024, 4:41 pm
Mradi wa TACTIC utakuwa na lengo la kusaidia Kutekeleza Miradi ya maendeleo katika jamii.
Na Sima Bingilek
Halmashauri ya Mji Mafinga ni moja kati ya Halmashauri 18 nchini zitakazonufaika na Mradi wa TACTIC kwa Awamu ya Tatu.
Timu ya Wataalamu kutoka OR- TAMISEMI kwenye Mradi wa TACTIC akiwemo Mtaalamu wa GIS Bi, Vainess Tarimo na Mchumi Ndugu Adam wametembelea Halmashauri ya Mji Mafinga lengo likiwa ni kutoa kushauri kuhusu Miradi iliyopendekezwa na Halmashauri na kuona changamoto na utatuzi wa changamoto hizo kabla ya kuanza utekelezaji wa Miradi hiyo kwa Timu ya Menejimenti.
TACTIC ni Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Miji ya Tanzania na Moja ya Malengo ya Miradi ya TACTIC ni kugusa wananchi wengi na Wananchi wa hali za kawaida, kuinua uchumi na kuboresha uwezo wa Taasisi katika Kutoa huduma bora kwa wananchi.
Wataalamu kutoka OR-TAMISEMI kwenye Mradi wa TACTIC wamefanya mazungumzo na kukagua baadhi ya barabara wakiwa na Timu ya Menejimenti ya Halmashauri ya Mji Mafinga ikiongozwa na Kaimu Mkurugenzi Ndugu Francis Magembe.
Halmashauri ya Mji Mafinga ilipendekeza Miradi ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, Ujenzi wa Stendi ya kisasa ya Mabasi na Soko la Mbao( Timber Market ).