Kihenzile awaita wawekezaji usafiri wa reli
5 March 2024, 8:40 pm
Na Mwandishi wetu
Wawekezaji wameshauriwa kujitokeza kwa wingi kuwekeza katika usafiri wa reli hapa nchini.
Wito huo umetolewa mkoani Mwanza na Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile ambaye ni Mbunge wa Mufindi Kusini wakati alipokuwa akizindua jukwaa la uwekezaji la reli.
Jukwaa hilo la siku mbili limeandaliwa na Shirika la Reli nchini(TRC).
Kihenzile amesema kuwekeza katika reli itasaidia katika kuleta maendeleo pamoja na kuinua sekta mbalimbali.
Amesema uwekezaji katika Reli ya Kisasa(SGR) utasaidia katika kujenga viwanda kwenye mikoa ya Mwanza, Kigoma pamoja na Tabora.
Ameongeza kuwa uwekezaji katika usafiri wa reli utasaidia katika kuongeza ukusanyaji wa mapato .
Amesema kupitia jukwaa la uwekezaji katika sekta ya reli utasaidia katika upatikanaji wa wawekezaji imara watakaoweza kuwekeza katika sekta hiyo.
Mkurugenzi wa Shirika la Reli nchini(TRC) Masanja Kadogosa amesema shirika hilo litatumia mkutano huo wa siku mbili kuelezea fursa mbali mbali zinazopatikana katika sekta ya reli.
Amesema Shirika lao limekuwa linafanya maboresho mbalimbali ya reli kuanzia Dar es salaam mpaka Tabora na Tabora kwenda Isaka.
Katika hatua nyingine amesema ujio wa reli ya kisasa utasaidia katika ujenzi wa viwanda mbali mbali kwenye maeneo ambayo reli imepita.