Kiwanda Cha Dark Earth Carbon kuanza uzalishaji wa mbolea ya asili Mufindi.
27 February 2024, 8:22 am
Na Hafidh Ally
Serikali Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa Inatarajia kuona uzalishaji wa mbolea ya asili unaotokana na mabaki ya mazao misitu unaanza katika kiwanda Cha Dark Earth Carbon.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Mheshimiwa Dkt. Linda Salekwa kwenye ziara ya Awamu ya pili ya Oparesheni viwandani katika Wilaya ya Mufindi kiwanda cha Dark Earth Carbone kilichopo Mafinga.
“ Tunatamani muanze uzalishaji katika kiwanda hiki cha kuzalisha mbolea ya Asili inayotengenezwa na mabaki ya mazao ya misitu, Serikali ipo pamoja na wawekezaji katika kuhakikisha mnapata mazingira mazuri ya uzalishaji bila kuvunja sheria za nchi na inatupa faraja kuona vijana wengi wa Kitanzania wanapata ajira”
Akitoa taarifa ya kiwanda hicho Mkurugenzi wa Uendeshaji Ndugu Amar Shanghavi amesema kiwanda hicho kilianza rasmi mwaka 2022 na uzalishaji ulianza mwaka 2023 kwa kuzalisha mbolea ya asili inayotokana na mabaki ya misitu ambayo yanapatikana kutoka kwa wakulima.
“Tunachosubiri kwa sasa ni majibu kutoka TARI ili sasa tuanze rasmi usambazaji wa Mbolea yetu, na upande wa Serikali tunaomba utambulisho ili tunapowafuata wakulima huko mashambani na kuamua kuanzisha mashamba darasa basi tuwe na barua rasmi kutoka Serikalini. Pia Suala la Ushuru tunaomba liangaliwe kwa upana wake” Mr. Amar Mkurugenzi wa uendeshaji.
Mkuu wa Wilaya akiwa ameambatana na Wataalamu kutoka Halmashauri ya Mji mafinga na Wataalamu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mufindi wamekagua miundombinu ya kiwanda na kutoa ushauri mbalimbali pamoja na kuchukua changamoto za wawekezaji hao.
Kiwanda cha Dark Earth Carbon kina jumla ya wafanyakazi 57 na kipo katika Halmashauri ya Mji Mafinga.