Rais Samia atoa ndege kwa Stars
13 November 2023, 11:19 am
Rais Samia Suluhu Hassan ametoa ndege kwa ajili ya kuisafirisha timu ya Taifa ya Soka, Taifa Stars kwenda Marrakesh kwa ajili ya mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Niger utakaochezwa ugenini Novemba 18, mwaka huu, nchini Morocco.
Timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars ambayo ipo Kundi E, pamoja na timu za Morocco, Zambia, Congo na Niger baada ya mchezo huo inarudi kucheza nyumbani na Morocco Novemba 21 mwaka huu. Fainali za Kombe la Dunia zitafanyika Marekani, Canada na Mexico.
Kupitia ukurasa wake mtandao wa X (zamani Twitter) Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa alichapisha maandishi na sauti akieleza kuwa Rais Samia ametoa ndege kwa ajili ya kuisafirisha Taifa Stars na kumshukuru.
“Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametoa ndege kwa ajili ya kuisafirisha timu ya Taifa ya soka ya Taifa Stars ambako itaumana na timu ya Taifa ya Niger katika kutafuta tiketi ya kufuzu michuano ijayo ya Kombe la Dunia”.
“Tunakushukuru sana Mheshimiwa Rais, sasa timu itasafiri kwa muda mfupi kwenda Marrakesh tarehe 16 Novemnba, 2023 na itarejea haraka tarehe 19 Novemba, 2023 baada ya mchezo wake wa tarehe 18 Novemba, 2023 dhidi ya Niger,” aliandika Msigwa.
Oktoba 04 mwaka huu wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikabidhi Sh milioni 500 kwa Taifa Stars ambazo ni ahadi ya Rais Samia aliyoitoa baada ya kufuzu kucheza AFCON mwaka 2023 yatakayofanyika Ivory Coast mapema mwaka 2024, Rais wa Shirikisho la Soka nchini Tanzania (TFF) Wallace Karia aliomba serikali kusaidia usafiri binafsi Taifa Stars kwenda kucheza Morocco dhidi ya Niger.
Baada ya Karia kuwasilisha ombi hilo Majaliwa alisema amelichukua huku akiongeza kusema: Wallace una wasiwasi na Rais wako? Hilo tu!! Nimelichukua.”
Nyota wa Taifa Stars wanaocheza soka nyumbani wapo hoteli ya Golden Tulip, Masaki, Dar es salaam na wameanza mazoezi ya viungo na wanaocheza nje wana tarajiwa kuanza kuwasili leo Jumatatu (Novemba 13).