Mafinga washinda tuzo saba mashindano UMISETA
9 June 2023, 7:52 pm
Na Frank Leonard
Halmashauri ya mji Mafinga imeshinda vikombe saba kwenye mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa wanafunzi wa Shule za Sekondari (UMISSETA) ngazi ya mkoa.
Mashindano hayo yaliyofanyika katika shule ya sekondari ya JJ Mungai ya mjini Mafinga yalishirikisha halmashauri zote tano za mkoa wa Iringa.
Akizungumza mara baada ya vikombe hivyo kukabidhiwa, mkuu wa Kitengo cha Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Halmashauri ya Mji Mafinga, Henry Kapella amevitaja vikombe vilivyochukuliwa na halmashauri yake kuwa ni katika ngoma, usafi na mpira wa wavu wanawake mshindi wa kwanza.
Vingine ni mpira wa miguu wanaume, mpira wa pete, mikono na meza-mshindi wa pili.
“Pamoja na mafanikio haya, halmashauri yetu imefanikiwa kuingiza wanafunzi 15 kati ya 80 wanaounda timu ya UMISSETA mkoa,” amesema.
Mwenyekiti wa wakuu wa shule mkoa wa Iringa (TAHOSA), Albert Mkollo amesema michezo inaweza kuchochochea uchumi na mapato ya eneo husika na kwa muktadha huo akawaomba walimu na wataalam wa halmashauri kuipa kipaumbele kwani inaweza kusaidia kuongeza mapato ya halmashauri na kujenga afya ya akili ya mwanafunzi.
Afisa Elimu Sekondari Stephen Shemdoe amesema ili kukuza tasnia hiyo, halmashauri yao imeandaa mafunzo kwa walimu wa michezo ukiwemo mchezo wa kikapu na itatenga bajeti ya michezo ya UMISSETA kupitia mapato yake ya ndani.
Akipokea vikombe hivyo Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mafinga, Apolinary Seiya ametoa pongezi kwa ushindi huo na kwa walimu wa michezo, Afisa Elimu Sekondari na wakuu wa Shule kwa michango yao iliyowezesha matokeo hayo pamoja na ya chakula kwa wanafunzi wakati wote wa kambi.
Amewataka walimu na wanafunzi waliochaguliwa katika timu ya UMISSETA mkoa kuhakikisha wanadumisha nidhamu na kucheza kwa bidii ili kurudi na ushindi wa taifa.