Washiriki Great Ruaha Marathon wahakikishiwa usalama ndani ya hifadhi
26 May 2023, 12:13 pm
Na Hafidh Ally
Washiriki wanaotarajia kushiriki mbio za Great Ruaha Marathon 2023 ambazo zitafanyika katika hifadhi ya taifa ya Ruaha, wamehakikishiwa kuwepo kwa usalama wakati wote wa mashindano hayo.
Akizungumza na Nuru FM mratibu wa shirika la Sustainable Youth Development Partnership (SYDP) linalojishughulisha na utoaji wa elimu ya afya, stadi za maisha na ujasiriamali kwa vijana, hifadhi na utunzaji wa mazingira, Hamim Kilahama amesema kuwa mbio hizo zinafanyika kwa ushirikiano kutoka Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) kupitia hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
“Kutakuwa na ulinzi wa kutosha kwa kuwatumia askari wa wanyama Pori ambao watahakikisha kuna usalama kuanzia darajani eneo la Ibuguziwa ili washiriki wasikutane na madhara, na hata hivyo mbio hizo zinafanyika kwa kutoka nje ya hifadhi” alisema Kilahama.
Amesema kuwa lengo la kufanya mbio hizo ni kuhamasisha shughuli za utalii pamoja na kutoa ujumbe wa kulinda vyanzo vikuu vya mto Ruaha ambao umekuwa muhimu katika hifadhi hiyo.
Aidha Kilahama amewataka wanaotaka kushiriki mbio hizo kujisajili katika zoezi linaloendelea kwa sasa kwa njia ya mtandao kupitia wavuti yao ya www.greatruahamarathon.co.tz
Mbio hizo zitakazofanyika Julai 8 za kilometa 5, 10, 21, na km 42 zitakwenda sambamba na matembezi ya kawaida hifadhini humo.