Serikali yasisitiza Huduma Ya Kujipima Vvu Mahala Pa Kazi Yaanza
14 January 2023, 7:52 am
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya imeanzisha huduma ya kujipima VVU mahala pa kazi ili kurahisisha upatikanaji wa huduma ya vipimo vya VVU kwa watumishi makazini hasa wanaume, ambapo hadi kufikia Desemba 2022 watu wapatao 96,231 wamepatiwa huduma ya JIPIME mahala pa kazi.
Hayo yamejiri Jijini Dodoma wakati wakati Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel akiwasilisha taarifa kuhusu kuhuisha na kujumuisha maswala ya UKIMWI mbele ya kamati ya kudumu ya Bunge ya masuala ya UKIMWI.
“Wizara imeanzisha huduma ya kujipima VVU (JIPIME) mahala pa kazi ili kurahisisha upatikanaji wa huduma ya vipimo vya VVU kwa watumishi sehemu za kazi hususani Wanaume. Hadi kufikia Desemba 2022 watu wapatao 96,231 wamepatiwa huduma ya JIPIME mahala pa kazi.” amesema Dkt. Mollel.
Sambamba na hilo amesema, hadi kufikia Desemba 2022 jumla ya vijana balehe 47,705 (Wavulana 20,329 na Wasichana 27,376) walifikiwa katika shule zipatazo 103 kupitia kampeni ya Kipepeo, huku akibainisha kuwa, Kampeni hii inatarajiwa kufanyika mwaka 2023 katika mikoa ya Dodoma, Singida, Morogoro, Tanga na Geita.
Ameendelea kusema kuwa, kwa mwaka 2022 Wizara kwa kushirikiana na TACAIDS na Wizara ya Elimu imeweza kutoa mafunzo ya elimu ya jinsia kwa walimu wapatao 5,033 nchini.
Pamoja na hayo, Dkt. Mollel amesema, hadi kufikia Desemba 2022 kuna vituo vitano (5) vya kutolea huduma za afya katika maeneo ya Geita Gold Mine (Geita), North Mara Gold Mine (Mara), Bulyanhulu Gold Mine Limited (Shinyanga), New Luika Gold Mine (Songwe) na Mererani (Manyara).
Amesema, huduma za VVU zinazotolewa katika migodi hiyo ni pamoja na Upimaji wa VVU, huduma za tiba na matunzo ikiwemo utoaji wa ARV, huduma za tohara, huduma za JIPIME, huduma za dawa kinga (PrEP) na magonjwa mengine ya ngono.
Kwa upande wa wakazi wanaokaa maeneo yasiyifikika kwa urahisi hususani visiwani, amesema, Wizara imekuwa ikitoa huduma za VVU na UKIMWI kwa njia ya huduma mkoba ngazi ya jamii na baadhi ya maeneo kama visiwa hususani Ziwa Vitoria Mkoani Mwanza huduma hii hutolewa kwa kutumia usafiri wa boti maalum (Fikia boat).
Aidha, Dkt. Mollel amesema, Kwa kipindi cha Januari hadi Desemba 2022 jumla ya kondomu 111,934,600 zilisambazwa nchini ili kuongeza mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI, huku kati ya hizo, kondomu 2,806,500 zimesambazwa katika Wizara na Taasisi mbalimbali.