Nuru FM

RC Dendego Amefufua Shamba La Chai Kijiji Cha Kidabaga Wilaya Kilolo

4 October 2022, 9:17 am

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Halima Dendego amelifufua shamba la Chai lenye hekta zaidi ya elfu 3,000 katika Kijiji cha Kidabaga Kilichopo kata ya Dabada Wilaya ya Kilolo ambalo halikufanya uzalishaji kwa zaidi ya Miaka 30.

 

Akiungumza katika mashamba hayo ya chai, akiongozana na Mbunge wa Jimbo la Kilolo Mh. Justine Nyamoga pamoja na Kamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya Kilolo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mh. Dendego amesema kuwa atahahakikisha anasimamia mashamba hayo ili baada ya miezi mitatu wakulima waweze kuvuna Chai.

 

Amesema kuwa serikali tayari imeweka zaidi ya Milioni Mia Tatu huku akiwaagiza maafisa ugani kusimamia vyema fedha hizo ili ziendane na thamani ya kazi ambayo itafanywa katika mashamba hayo ya Chai.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kilolo Mh. Justine Nyamoga amesema kuwa Kufufuliwa kwa zao la Chai katika Jimbo lake kutasaidia kukuza uchumi wa Kilolo kuanzia kwa Mkulima Mmoja mmoja huku akiishukuru wizara ya Kilimo kwa kukubali maono ya kufufua zao hilo la kiuchumi.

 

Mh. Nyamoha amesema kuwa katika jimbo la kilolo kuna maeneo mengi ambayo yanafaa kwa kilimo cha chai kwa kuwa inastawi vizuri kwa sababu kuna mvua nyingi.

 

“Kuna maeneeo kama Kata ya Ng’uruwe, idete, ukwega, Kising’a, ukumbi, Ng’anga’ange, Mtitu, Boma la Ng’ombe, Kimara na baadhi ya maeneo ya ukanda wa ilula kuna vijiji vya ikokoto ambavyo vina maeneo mazuri sana kwa kilimo cha chai hivyo ni fursa kwa wawekezaji kuja kuwekeza katika zao hili” alisema Nyamoga

 

Kwa upande wake Afisa Kutoka Wizara ya Kilimo Bahati Majaliwa Yusuph amesema kuwa Wizara Ya Kilimo Kwa Kushirikiana Na Mradi Wa Agriconet Wametoa Zaidi Ya Milioni 300 Ili Kuzindua Na Kuboresha Sehemu Ya Kiwanda Cha Dabaga Ambacho Kitachakata Mazao Hayo Kwa Hatua Za Awali.

 

Awali Mkurugenzi  Mkuu wa Bodi ya Chai Tanzania Bw. Nicholas Mauya amesema kuwa Bodi ya Chai imekuwa ikishirikiana kwa karibu na Ofisi ya Mbunge Justine nyamoga kuhakikisha wanatimiza ndoto ya kuzalisha Chai hiyo ambayo ilisimama uzalishaji kwa zaidi ya miaka 30.

 

Nao baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Kidabaga Wilaya ya Kilolo Wameshukuru Mbunge wao kwa kuwasaidia kuja na hoja ya kufufua zao la chai kwa kuwa litawasadia kukua kiuchumi na kufikia malengo yao.

MWISHO