Serikali yatenga Bil. 3 ujenzi Hospitali ya rufaa
19 September 2022, 4:20 pm
Serikali, imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 3 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel hii leo Septemba 19, 2022 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum, Bupe Nelson Mwakang’ata kuhusu ujenzi wa Hospitali hiyo.
Dkt. Mollel amesema kuwa, Serikali imetenga kiasi cha Shilingi Milioni 900 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya kutolea huduma katika Hospitali ya sasa ambapo majengo yake ni chakavu.
Aidha, amesema kuwa Serikali inaendelea kufanya maboresho katika Sekta ya Afya kwa kuajili watumishi wapya na kutoa fursa za elimu kwenye fani za mbalimbali za Afya ikiwemo taaluma za kibingwa.
Amebainisha kuwa, Wizara imepeleka kusoma jumla ya madaktari watano kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa, ambao ni madaktari wawili wanasomea upasuaji, daktari mmoja anasomea upasuaji wa Mifupa (Orthopaedics), Daktari mmoja anasomea magonjwa ya dharula (EMD) na daktari mmoja anasomea kinywa, sikio na koo (ENT).
Dkt. Mollel amesema, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa hadi sasa ina jumla ya madaktari bingwa watano wa fani za Afya ya mama na uzazi (Obsy/gyn) wawili, magonjwa ya watoto (paediatric) wawili pamoja na daktari bingwa wa magonjwa ya ndani (physician) mmoja.