Waziri Mkuu Majaliwa aagiza Wabadhirifu MSD wachukuliwe hatua
10 May 2022, 6:36 am
Wziri Mkuu Kassim Majaliwa amefanya ziara katika Bohari ya Dawa (MSD) na kuagiza watu wote waliohusishwa na tuhuma za ubadhirifu zilizoainishwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wachukuliwe hatua.
Majaliwa amesema hoja zote zilizotolewa katika ripoti ya CAG lazima zifanyiwe kazi na tayari Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (TAKUKURU) imeanza kufanyia kazi hoja zote zilizotolewa kuhusu MSD.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Mei 09, 2022) wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa MSD baada ya kutembelea viwanda vya kutengeneza barakoa na dawa vilivyopo katika eneo la MSD, Keko jijini Dar es salaam.
Akizungumzia kuhusu baadhi ya hoja za CAG, Waziri Mkuu amesema MSD ilifanya ununuzi wa vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni tisa (9) bila ya mikataba halali jambo ambalo si sahihi.
Pia, Waziri Mkuu amesema taasisi hiyo ilifanya malipo yenye thamani ya shilingi bilioni 3.52 kwa wazabuni sita (6) bila ya kufuata utarabu na wala kuitaarifu bodi ya zabuni ya MSD.
Waziri Mkuu amesema MSD ilifanya zabuni 23 zenye thamani ya shilingi bilioni 8.55 zilifanywa nje ya Mfumo wa Ununuzi wa TANeps unaosimamiwa na PPRA kinyume na matakwa ya sheria ya ununuzi.
“MSD ilifanya malipo ya awali kiasi cha shilingi bilioni 14.89 kwa wazabuni watano (5) bila ya mikataba yoyote au makubaliano mengine ambayo yanabainisha msingi wa malipo ya awali.”
Amewataja wazabuni hao kuwa ni Keko Pharmaceutical Industry; Wakala wa Huduma za Ununuzi Serikalini; Nakuroi Investment Company Ltd.; Technical Services and General na Wide Spectrum (T) Ltd.
Waziri Mkuu amesema taasisi hiyo iliendesha mchakato wa ununuzi na kutoa mkataba wa kusambaza “Liquid Syrup” wenye thamani ya shilingi milioni 898 bila ya kushirikisha Bodi ya Zabuni ya MSD.
Amesema taasisi hiyo ilitumia kiasi cha shilingi milioni 215 kwa ajili ya kugharamia posho ya watumishi watatu waliokwenda China kwenye majadiliano ya kuleta mashine za dialysis kwa siku 61.
Amesema katika idara ya manunuzi kumebainika kuwepo kwa watumishi ambao si wataalamu, hivyo ameagiza wote 16 ambao si wataalamu waondolewe na kuwekwa watumishi wenye taaluma hiyo.
Mheshimiwa Majaliwa pia amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa MSD, Mavere Tukai afanye tathmini ya utendaji ndani ya MSD na achukue hatua pale atakapobaini kuwepo na dosari. “Ni muhimu kuimarisha eneo la ufuatiliaji.”
Kwa upande wake, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ametumia fursa hiyo kumshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuhakikisha Watanzania wanaendelea kupata dawa.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa MSD, Mavere Tukai alizitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili taasisi hiyo kuwa ni pamoja na kuwepo na usiri wa bei za bidhaa za afya zinazoamuliwa na wasambazaji walioingia mikataba za wazalishaji.
Pia, changamoto nyingine aliyoitaja ni kutokuwepo kwa mfumo wa kupata taarifa za uhakika na uchambuzi wa kina wa masoko ya bidhaa bora na za bei nafuu pamoja na kuwepo kwa udhaifu katika kitengo cha manunuzi.
Alisema tayari taasisi imeweka mikakati ya kutatua changamoto hizo ikiwa ni pamoja na kukijengea uwezo kitengo cha manunuzi, kubadilisha mfumo mzima wa ununuzi kuanzia wazalishaji, intelijensia na tafiti za bei na masoko na mahusiano na washitiri.
Mkakati mwingine alioutaja ni kupitia upya muundo wa MSD pamoja na rasilimali watu kwa sababu tayari muundo ulioko sasa umeonesha changamoto hivyo ni lazima ufumuliwe.