Polisi kuchunguza kifo cha Padri Kangwa
20 April 2022, 7:37 am
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema linaendelea na uchunguzi wa tukio la kifo cha Paroko wa Parokia ya Mbezi Mshikamano, Padri Francis Kangwa aliyekutwa ndani ya tenki la maji akielea.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro katika taarifa yake, amesema kuwa uchunguzi wa awali kwa kushirikiana na mamlaka nyingine zimeonyesha dalili kuwa padre huyo ambaye ni raia wa Zambia anaweza kuwa amejiua.
Padri huyo alikutwa amefariki ndani ya tenki kubwa la maji lililopo nyuma ya nyumba ya makazi ya mapadri Mtaa wa Sokoine katika jengo la Ottoman jijini Dar es Salaam.
“Padri huyo alifika katika kanisa la St. Joseph lililopo mtaa wa Sokoine Aprili 12, 2022 kwa ajili ya ibada maalum, na mara baada ya ibada hiyo alielekea kwenye makazi ya Mapadri kujipumzisha lakini hakuonekana mpaka Aprili 15 alipokutwa amefariki eneo hilo” ilisema taarifa hiyo.
“Uchunguzi wa awali kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za kiuchunguzi unaonesha dalili kwamba Padri huyo anaweza kuwa amejiua” imeeleza taarifa hiyo.
Hata hivyo taarifa hiyo imeeleza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kubaini sababu halisi iliyopelekea kifo cha Padri huyo.
Padri Francis Kangwa enzi za uhai wake
Kifo cha Padri Kangwa Kilitangazwa awali na paroko msaidizi Padri Louis Mtamati siku ya Ijumaa baada ya Ibada ya ijumaa Kuu ambapo waumini wake walianza kuhoji juu ya utata wa kifo chake wakati huzuni na simanzi vikitawala ikisemekana kuwa alikua miongoni mwa walioashiriki maandalizi ya sikukuu ya pasaka katika kanisa lake.
Tangu alipoingia katika kanisa hilo, Padri Kangwa Juni 18, 2017, ndiye aliyefanikisha ujenzi wa kanisa hilo na kulifanya kuwa parokia kamili lakini ameacha ujenzi wa nyumba za mapadri katika kanisa hilo.
Baada ya Uchunguzi wa Kipolisi na kukabidhiwa Mwili, viongozi wa parokia hiyo wamepanga kufanya maziko katika Parokia ya Mtakatifu Yohane II Mbezi Mshikamano na atakayeongoza maziko hayo ni Askofu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Yuda Thadeus Ruwai’ch.