Iruwasa Wilaya ya Kilolo kukabidhi bajeti kwa Balozi Isabela Kupitia DC Magiri ya kupeleka Maji kwa walemavu Lulanzi
24 March 2022, 5:19 pm
Mamlaka ya Maji na usafi wa Mazingira IRUWASA Wilaya ya Kilolo inatarajia kuandaa bajeti na kuipeleka kwa Mkuu wa Wilaya yenye lengo la kupeleka huduma ya maji katika Familia ya walemavu watatu wa kijiji cha Lulanzi Wilayani Kilolo.
Bajeti hiyo ambayo inaandaliwa na Wataalamu Kutoka Iruwasa Wilayani Kilolo itapelekwa siku ya ijumaa tarehe 25/3/2022 kwa Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Peresi Magiri na kisha kuiwasilisha kwa Balozi wa Utalii Nchini Bi Isabella Mwampamba ambaye atashirikiana na wafanyabiashara, Kampuni , Taasisi za dini, Taasisi za serikali na zisizo za kiserikali, Vyuo na wadau wengine wa maendeleo kuhakikisha maji yanafika katika Familia hiyo.
Akizungumzia kuhusu Mchakato huo wa kuandaa bajeti ya kupeleka maji kwa familia hiyo Meneja wa Iruwasa Wilaya ya Kilolo Eng Paul Mboka amesema kuwa kwa kushirikiana na wataalamu wa maji na ujenzi wataandaa bajeti ambayo itakuwa rahisi kupeleka huduma ya maji ambayo imekuwa changamoto ya muda mrefu kwa walemavu hao.
Eng. Mboka ameongeza kuwa lengo la kuandaa bajeti hiyo ni kuhakikisha familia hiyo inapata huduma ya maji huku akiwasihi wadau wengine kujitoa na kumuunga Mkono Balozi Isabella na washirika wake katika kampeni yake.
Hatua hiyo imekuja siku moja bada ya Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Peresi Magiri Kufika katika kijiji cha Lulanzi akiwa na timu ya watalamu kutoka Iruwasa Wilayani kwake kuwatembelea walemavu ambao walimuomba Balozi Isabella kuwapatia huduma ya maji katika nyumba yao.
Naye balozi wa Utalii Nchini Isabela Mwampamba ameahidi kufika tena katika kiijiji hicho siku ambayo zoezi la uwekaji wa huduma ya maji katika familia hiyo yenye walemavu akiwa na wanawake ambao wameahidi kuchangia fedha kwa ajili ya Mradi huo.
Aidha Bi Isabella amewasihi Watanzania kushiriki kuchangia fedha mara baada ya kupewa gharama za kupeleka huduma ya maji katika familia hiyo.