Dc Kilolo Aunga Mkono Kampeni Ya Balozi Isabela Ya Kuisaidia Familia Ya Walemavu Lulanzi
23 March 2022, 4:55 pm
Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Peres Magiri amewatembelea familia ya walemavu watatu waliopo katika kijiji cha Lulanzi ikiwa imepita siku chache baada ya Balozi wa Utalii Nchini Tanzania Bi. Isabela Mwampamba kufika na kuanza mchakato wa kutatua changamoto zinazowakabili.
Changamoto zinazowakabili familia hiyo ni pamoja na jiko lao kuvunjika, kutokuwa na shedi ya kupumzikia pamoja na ukosefu wa huduma ya maji ambayo imekuwa ni changamoto kubwa kwa familia hiyo.
Akizungumza mara baada ya kufika leo kijijini hapo akiwa na Timu ya wataalamu Kutoka Mamlaka ya Maji safi na usafi wa Mazingira Iruwasa, Mkuu wa Wilaya huyo Mh. Magiri amesema kuwa alipata taarifa za ujio wa Balozi Isabella na mkakati ambao waliuweka ili kutatua changamoto hizo.
Mh. Magiri amesema kuwa amefika akiwa na Wataalamu wa Iruwasa na wamefanya tathmini ya kuweka huduma ya maji ambapo wamekubaliana na wanakijiji wa eneo hilo kushiriki kwa kutoa nguvu kazi ya kuchimba Mtaro wa kupitisha mabomba ya Maji mpaka katika familia hiyo.
Hata hivyo ameongeza kuwa amewasiliana na Balozi Isabella na wamekubaliana kufanya tathimini ya gharama za ujenzi wa jiko, shedi na gharama za kuweka maji kisha kumpatia ili waanze mchakato wa kuchangishana fedha kutoka wadau wake.
Katika hatua nyingine Mh. Peresi Magiri amempongeza balozi Isabella kwa kuwatembelea walemavu hao na kutambua changamoto zinazowakabili huku akiahidi kushirikiana naye kuhakikisha azma aliyoianzisha inatekelezeka kwa ufanisi.
March 20 mwaka huu Balozi wa Utalii Nchini Bi. Isabella Mwampamba Yupo Mkoani Iringa, akiwa na wanawake ambao ni wadau wa utalii Nyanda za juu kusini kwa kushirikiana na wizara ya utalii kupitia bodi ya utalii kanda ya iringa walifanya utalii wa kutembelea vivutio vilivyopo Mkoani Iringa sambamba na kuikumbuka jamii kwa kutoa misaada katika familia hiyo yenye walemavu watatu.